1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bomu la kujitoa muhanga laua 58

Admin.WagnerD11 Februari 2016

Wanawake wawili katika kambi ya wakimbizi, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wamejitoa muhanga na kusababisha mauaji ya kiasi ya watu 58, maafisa wa polisi na idara ya uokozi wamethibitisha tukio hilo.

Eneo la shambulio mjini Maiduguri.
Eneo la shambulio, mjini Maiduguri.Picha: Getty Images/AFP/Stringer

Mwanamke mwingine wa tatu alitiwa mbaroni na kutoa taarifa za mipango ya shambulizi lingine la mabomu ambazo zilisaidia kuimarisha ulinzi katika kambi hiyo.

Hadi sasa kiasi cha watu 78 wanatibiwa kutokana na majeraha waliyoyapata katika shambulizi hilo lililotokea Jumanne wiki hii katika kambi hiyo ambayo wanaishi watu takriban 50,000 ambao wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kitisho pamoja na mashambulizi yanayofanywa na kundi hilo la Boko Haram.

Hii ni kwa mujibu wa maafisa wa Afya katika mji wa Maiduguri ambao ni mji mkubwa kuliko yote katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambako ndiko asili ya kundi hilo la itikadi kali.

Maafisa hao walitoa taarifa hizo kwa sharti la kutotajwa majina kama ilivyokuwa kwa wale wa kitengo cha uwokozi, wakisema kuwa hawana ruhsa ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Maafisa wa kitengo kinachohusika na masuala ya dharura walisema miili ya watu 51 ilizikwa hapo jana katika eneo la Dikwa kilomita 85 Kaskazini Mashariki mwa Maiduguri. Shirika linalohusika na kusambaza habari nchini Nigeria lijulikanalo kama PR Nigeria hapo jana liliwakariri maafisa wa Afya pamoja na wale wa uwokozi wakisema idadi ya watu waliouawa katika tukio hilo kuwa ni 58.

Cameroon wapata tishio la Boko haramPicha: picture-alliance/dpa/N. Chimtom

Maafisa wanasema mawasiliano hafifu kwa njia ya simu yalisababisha kuchelewa kufika kwa taarifa za shambulizi hilo.

kundi la Boko Haram limeendelea kutishia hata nje ya mipaka ya Nigeria.

Kundi la itikadi kali la Boko Haram ambalo limedumu katika kipindi cha miaka sita na kitisho chake kusambaa mipakani mwa Nigeria hadi sasa limesababisha vifo vya watu 20,000, na kuwalazimisha watu milioni 2.5 kuyahama makazio yao.

Wakati huohuo huko Kaskazini mwa Cameroon , watu wawili wanaoaminika kutokea nchini Nigeria walijitoa muhanga na kuwaua watu 10 huku wengine 40 wakijeruhiwa katika kijiji kimoja cha mpakani nchini humo.

Kundi hilo la Boko Haram pia linadaiwa kufanya mashambulizi katika mataifa ya Chad na Niger.

Tangu wakati majeshi katika mataifa ya Nigeria, Chad na Cameroon yalipofanikiwa kuwaondosha wanamgambo wa kundi hilo la Boko Haram kutoka katika maeneo ya miji na vijiji ambako walikuwa tayari wanaonekana kuotesha mizizi ya itikadi zao , wanamgambo hao sasa wamekuwa wakielekeza mashambulizi yao wakiyalenga maeneo yenye watu wengi kama vile misikiti na masoko.

Mwandishi : Isaac Gamba/ APE/ DPAE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi