1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bomu laua watu 3 katika kambi ya wakimbizi DRC

13 Februari 2024

Watu watatu wamekufa baada ya kutokea mripuko wa bomu, katika kambi ya wakimbizi, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku Afrika Kusini ikiridhia kupeleka wanajeshi wake 2,900 katika eneo hilo.

Mapigano ya DR Congo yaendelea mashariki | Kambi ya IDP ya Rusayo
Picha hii, iliyopigwa Oktoba 2, 2023, inaonyesha soko la kambi ya IDP ya Rusayo, makazi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, viungani mwa Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Masuala yote hayo yanatokea katika kipindi ambacho kimegubikwa na mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na waasi wa M23. Vikosi vya serikali na waasi wa M23 waliendeleza mapigano yao mchana wa Februari 12, katika eneo la Sake, upande wa Magharibi ya mji mkuu wa Goma.

Kwa mujibu wa shirika moja la kiraia, mapigano hayo yameendelea hadi jioni ya kuamkia Jumanne. Shirika hilo limelilaumu kundi la M23 kuishambulia kambi ya Zaina, na kusababisha vifo vya watu watano na raia wengine 15 wamejeruhiwa.

Vifo vitatu na watu wengine 18 wamejeruhiwa

Picha iliyopigwa Oktoba 2, 2023, inaonyesha kambi ya IDP ya Rusayo, makazi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, viungani mwa Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Chanzo kutoka katika jitihada za matibabu, kiliripoti kuwa majeruhi watatu kati ya 18 walipoteza maisha katika shambulio hilo. Mamlaka katika maeneo hayo ilitoa onyo kuwa mapigano ambayo yanaendelea yanaweza kusababisha wimbi jipya la watu kuhama makazi yao.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na msemaji wa serikali, Patrick Muyaya kupitia mtandao wa X  zamani Twitter, amelishutumu jeshi la Rwanda kwa kuripua bomu na kuongeza kuwa watu wanane wamejeruhiwa vibaya.

Raia waendelea kuukimbia mji wa Sake

Mapigano yamezidi kati ya M23 na jeshi la Kongo miongoni mwa makundi yenye nguvu kati ya makumi ya makundi yenye silaha yanayozunguka eneo la mashariki lenye matatizo kwa muda mrefu.

Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya raia kuukimbia mji wa Sake, eneo la kimkakati la barabara ya kuelekea Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini. Kundi la M23 limeteka maeneo makubwa ya jimbo hilo tangu lilipotoka katika hali ya utulivu mwishoni mwa 2021, eneo ambalo limekumbwa na miongo kadhaa ya machafuko na vita vya kikanda.

Afrika Kusini yakubali kutimiza ahadi ya kupela wanajeshi 2,900 DRC


Katika hatua nyingine Afrika Kusini imetimiza ahadi iliyotoa kwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya kutoa wanajeshi wapatao 2,900 kwenda kupambana na makundi yenye silaha yanayopigana na jeshi huko Mashariki ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Askari wa Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) wakiongozana na waandishi wa habari katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la M23 huko Bunagana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Aprili 19, 2023.Picha: Glody Murhabazi/AFP

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais imesema, jeshi hilo litahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Disemba 15, 2024 na itagharimu kiasi cha randi billioni 2. SADC yenye nchi wanachama 16 iliidhinisha mpango wa kijeshi katika kusaidia kuimarisha hali ya utulivu nchini Kongo mwezi Mei mwaka 2023.

Kongo nchi kinara kwa usambazaji wa Kobalti na uzalishaji wa madini ya shaba barani Afrika, kwa miongo kadhaa imekumbwa na migogoro hususani upande wa mashariki mwa taifa hilo, na kupelekea vifo na uharibifu wa mali, huku zaidi ya watu milioni 7 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Majukumu ya walinzi wa amani wa SADC katika eneo la mashariki la DRC

Kikosi hicho kilichotumwa na SADC kina jukumu la kuiunga mkono Kongo na kusaidia kupambana dhidi ya makundi ya waasi wenye silaha. Jeshi hilo linajumuisha wanajeshi kutoka nchi za Malawi, Afrika Kusini na Tanzania.

Soma zaidi:Wageni wote wanaoingia na kutoka mji wa Goma kuandikishwa

Kutumwa kwa wanajeshi hao kumekuja wakati huu ambao jeshi la Kongo linapambana na waasi wa M23 ambapo mashambulizi yao katika siku za hivi karibuni yameongeza waiwasi mkubwa.

Chanzo: AFP/RTR

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW