Bomu lawaua askari wawili wa kulinda amani Mali
4 Juni 2022Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema shambulio hilo limetokea karibu na mji wa Douentza katika barabara inayoelekea Timbuktu. Aidha, Dujarric ameongeza kuwa mashambulizi hayo yanalenga kutatiza maisha ya watu wa Mali na kuvuruga usalama. "Hili ni tukio la sita ambapo msafara wa walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa umelengwa tangu Mei 22", alisema Dujarric.
Ameongeza kuwa pamoja na changamoto hizo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea na kazi yao kwa mujibu wa mamlaka yao ya Baraza la Usalama, akitolea mfano ushiriki wa MINUSMA katika ukarabati wa hivi karibuni wa madaraja mawili yaliyoharibiwa katika eneo moja.Ujerumani yarefusha muda wa jeshi lake nchini Mali
Kumekuwa na mkururo wa mashambulizi dhidi ya askari wa kulinda amani na wafanyakazi wa misaada ya kiutu. Askari wawili waliauwa na tisa kujeruhiwa katika shambulio la kushtukiza Kaskazini mwa Mali siku ya Alhamis. Katika tukio la Alhamisi, mkokoteni uliokuwa ukitoka sokoni ulikanyaga bomu dogo katika wilaya ya Waya, na kuua raia watano na kujeruhi vibaya mtu wa sita aliyefariki siku ya Ijumaa.
Naye msemaji wa ujumbe wa MINUSMA Olivier Salgado amelaani shambulizi hilo. Amesema walinda amani hao wa Misri walikuwa wakisindikiza magari kadhaa ya Umoja wa Mataifa yakiandamana na msafara wa lori za raia zilizobeba mafuta.
Siku ya Jumatano, mfanyakazi wa kofia ya bluu wa Jordan aliuawa katika shambulio lililolenga msafara wake mjini Kidal, Kaskazini mwa Mali. Kikosi cha MINUSMA chenye askari 13,000 kilicho na jukumu la kulinda amani Mali, ni mojawapo ya kikosi kikubwa cha operesheni za Umoja wa Mataifa.
Tangu kuundwa kwake mwaka 2013, kimepoteza askari wapatao 174. Eneo la Mali ya kati limegubikwa na vurugu za wanamgambo ambazo zimeanea kutoka Kaskazini mwa nchi na hadi nchi jirani za Burkina Faso na Niger. Maelfu ya raia na wanamgambo wameuawa huku mamia wakiyakimbia makaazi yao.
Ripoti mbili zilizochapishwa wiki hii, moja kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterresna nyingine kutoka kitengo cha haki za binadamu cha MINUSMA, zilielezea hofu kutokana na kuongezeka kwa ghasia katikati mwa Mali.
Wakati huohuo muungano wa wanamgambo wenye makao yake makuu nchini Mali wenye mafungamano na Al-Qaeda wamedai kuhusika na shambulizi nchini Togo mwezi uliopita, kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la ufuatiliaji wa masuala ya Ujasusi la SITE.