BONN: Mgomo mkuu wa wafanyakazi wa Deutsche Telekom
11 Mei 2007Matangazo
Nchini Ujerumani hii leo wafanyakazi wa shirika la simu “Deutsche Telekom” wamepanga kufanya mgomo mkuu wa kwanza katika historia ya shirika hilo.Chama cha wafanyakazi “Verdi” kimesema asilimia 96 ya wanachama wake wamepiga kura kugoma kazi.Mgomo huo umeitishwa kupinga mpango wa “Telekom” unaotazamia kupanga upya nafasi 50,000 za ajira.Kuambatana na mpango huo wafanyakazi hao 50,000 watapaswa kufanya kazi muda mrefu zaidi kwa mishahara itakayokuwa midogo zaidi.Uamauzi huo umepitishwa baada ya shirika la “Telekom” kutangaza kuwa faida katika robo ya mwanzo ya mwaka huu imepunguka kwa kama asilimia 50.Sababu kuu ni kwamba maelfu ya watu wamehamia makampuni mengine ya simu yaliyo na bei nafuu, kulinganishwa na “Telekom”.