1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya mwisho ya uhamisho

1 Septemba 2023

Ijumaa mosi ni siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho wa wachezaji barani Ulaya, timu katika Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga zimekuwa mbioni kuviimarisha vikosi vyao.

Italia Kandanda Serie A |  Udinese Calcio - Juventus FC
Nahodha wa zamani wa Juventus Leonardo BonucciPicha: Ettore Griffoni/LiveMedia/ipa/picture alliance

Union Berlin

Berlin ambao wamefuzu kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya wamekamilisha usajili wa beki wa zamani wa Italia na timu ya Juventus Leonardo Bonucci mwenye miaka 36.

Bonucci ambaye ameshinda mataji chungunzima na ana uzoefu tele, ameondoka Juventus ya Italia baada ya kuambiwa na kocha Massimiliano Allegri kwamba hayuko kwenye mipango yake ya msimu huu.

Union wanatarajia kwamba atawaongezea nguvu hasa kwenye safu yao imara ya ulinzi kuelekea mechi za Champions League

Bayern Munich

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanaripotiwa kwamba wana matumaini ya kukamilisha kumnunua kiungo mkabaji wa Ureno anayeichezea klabu ya Fulham Joao Palinha.

Kocha wa Bayern Thomas Tuchel anaona kuna mapungufu katika nafasi hiyo kwenye kikosi chake kwa kuwa wachezaji alio nao kama Joshua Kimmich, leon Goretzka na Konrad Laimer wanapenda kwenda mbele na kufanya mashambulizi.

Ikumbukwe Bayern tayari msimu huu waliwasajili Harry Kane kutoka Tottenham Hotspur, Kim Min-jae beki wa kati wa Korea Kusini kutoka Napoli, Raphael Guerreiro aliyejiunga nao bila dau lolote kutoka Borussia Dortmund na Konrad Laimer aliyetokea RB Leipzig.

Borussia Dortmund

Borussia Dortmund nao wanaripotiwa kukamilisha usajiliwa Niclas Füllkrug kutoka Werder Bremen kwa dau la yuro milioni 15. Dortmund wanatarajia kwamba Füllkrug ambaye mtindo wake wa uchezaji unadaiwa kuwa ni wa kandanda la zamani, ataiamsha Dortmund kutoka usingizini kwani imekuwa na michezo miwili mibovu ya ufunguzi wa ligi.

Niclas Füllkrug amejiunga na Dortmund kutoka Werder Bremen Picha: Bratic/nordphoto GmbH/picture alliance

Dortmund tayari wameshawasajili Marcel Sabitzer na Felex Nmecha pamoja na Bensebaini kutoka Borussia Mönchengladbach.

Kwengineko inaripotiwa kwamba Eintracht Frankfurt huenda wakampoteza mshambuliaji wao Randal Kolo Muani ambaye hapo Alhamis alikataa kufanya mazoezi kwa ajili ya kushinikiza kuhamia Paris Saint Germain.

Kolo Muani ambaye tayari ashawafungia Frankfurt goli katika ligi msimu huu, ni mmoja wa wachezaji wanaonyatiwa na miamba hao wa Ufaransa na huenda akajiunga na PSG kabla makataa ya usiku wa Ijumaa ya uhamisho.