1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Borell aonya Lebanon kuingizwa vitani Mashariki ya Kati

6 Januari 2024

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell ametoa hadhari leo dhidi ya kutanuka kwa mzozo wa Mashariki ya Kati baada ya kuongezeka makabiliano kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa nchini Lebanon.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell. Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Akizungumza na waandishi habari akiwa pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Lebanon mjini Beirut, Borell amesema ni muhimu sana kuepusha Lebanon kujiunga na vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas huko Ukanda wa Gaza. Mwanadiplomasia huyo amesema  hakuna upande utakaoshinda iwapo kanda nzima ya Mashariki ya Kati itatumbukia vitani.

Matamshi yake yanafuatia kuongezeka mapambano kwenye eneo la mpaka kati ya kundi la Hezbollah na jeshi la Israel. Hali ya kutanuka kwa uhasama imeshuhudiwa zaidi tangu kuuwawa kwa naibu kiongozi wa kundi la Hamas katika shambulizi la droni mjini Beirut ambalo Hezbollah na washirika wake wanashuku lilifanywa na Israel.