1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson aaga, Truss kuwa waziri mkuu rasmi

6 Septemba 2022

Liz Truss hii leo anatarajiwa rasmi kuwa waziri mkuu mpya wa Uingereza baada ya hapo baadaye kwenda Scotland kukutana na Malkia Elizabeth na kisha kuteua baraza la mawaziri.

Großbritannien | Liz Truss
Picha: Phil Noble/REUTERS

Waziri mkuu anayeondoka Boris Johnson naye anakwenda Scotland kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia. 

Liz Truss jana alifanikiwa kumuangusha mpinzani wake Rishi Sunak kwenye kinyang'anyiro cha kuongoza chama kikongwe nchini humo cha Conservative, na kukata tiketi ya moja kwa moja ya kuwa waziri mkuu.

Truss, anaingia ofisini huku taifa hilo likikabiliwa na changamoto lukuki za kiuchumi kuanzia mzozo wa nishati hadi mfumuko wa bei ambavyo kwa pamoja imechangiwa na vita vya Ukraine na Urusi, janga la UVIKO-19 na Brexit. Mfumuko wa bei nchini humo umeongezeka kwa asilimia 10, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo minne na Benki Kuu ikibashiri mzozo huo utaongezeka hadi asilimia 13 ifikapo mwezi Oktoba.

Lakini Truss ameahidi kwamba kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kupunguza kodi na kanuni ili kusaidia mchakato wa ukuaji wa uchumi. Kwenye hotuba yake ya jana, Truss aliahidi kuisaidia Uingereza kukabiliana na mzozo wa uchumi na mapema leo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kwamba anapanga kutoa kifurushi cha pauni bilioni 40 kwa ajili ya kunusuru biashara.

Soma Zaidi: Mpambano wa kuwania uongozi Uingereza waanza rasmi

Aidha Truss ameahidi kuendelea kuisaidia Ukraine na kuongeza mchango wa Uingereza katika bajeti ya ulinzi kwa zaidi ya asilimia 2 hadi 3 ya pato jumla la ndani la Taifa. 

Boris Johnson ameahidi kumsaidia waziri mkuu mpya Liz Truss kupambana na changamoto za kiuchumi nchini Uingereza.Picha: Toby Melville/REUTERS

Waziri Mkuu anayeondoka Boris Johnson ambaye baadaye atakutana na Malkia Elizabeth kumkabidhi barua ya kujiuzulu amesema katika hotuba yake ya mwisho kabla ya kuondoka kwamba atahakikisha anamsaidia Truss kwa kila namna na kuongeza kwamba anaamini ataweza kuwasaidia Waingereza kujiondoa kwenye hali ngumu wanayoipitia sasa.

''Huu ni wakati mgumu kiuchumi. Huu ni wakati mgumu kwa familia hapa nchini. Tunaweza, tutapita na tutatokea upande mwingine tukiwa imara zaidi. Nawaambia wahafidhina wenzangu, wakati wa siasa umekwisha jamani, ni wakati wa sisi sote kumuunga mkono Liz Truss na timu yake na mpango wake na kujitoa kwa ajili ya watu wa nchi hii, kwa sababu ndivyo watu wa nchi hii wanavyotaka, hicho ndicho wanachohitaji na wanachostahili.'' alisema Johnson.

Ametoa hotuba yake mapema leo nje ya ofisi za waziri mkuu zilizopo mtaa wa Downing jijini London.

Ikumbukwe Boris Johnson alitangaza kujiuzulu Julai 7, kufuatia shinikizo kutoka ndani na nje ya chama chake baada ya ukosoaji kuhusiana na usimamizi mbovu kwenye vita dhidi ya janga la UVIKO-19, msururu wa kashfa zilizohusisha ofisi yake na madai ya kumdanganya Malkia na bunge. Julai 23, 2019 alichaguliwa kukiongoza chama cha Conservative, baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Theresa May kujiuzulu. Kwenye utawala wake, Johnson amefanikiwa pamoja na mengine kuufanikisha mchakato wa kuiondoa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya ama Brexit.

Soma Zaidi: Johnson kitanzini baada ya mawaziri zaidi kuachia ngazi

Mashirika:DW/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW