1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson afanya kikao na baraza lake la mawaziri

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
25 Julai 2019

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Boris Johnson leo amekutana na baraza lake jipya la mawaziri, wakati  ambapo anakabiliwa na kazi ngumu ya kuileta nchi yake pamoja iliyogawika kwa kiwango kikubwa.

England, London: Boris Johnson hält erste Kabinettssitzung
Picha: Reuters/A. Chown

Johnson ameahidi kuuondoa mkwamo wa Brexit uliosababisha kujiuzulu kwa waziri mkuu wa hapo awali Theresa May. Baadae Waziri Mkuu huyo mpya atatoa taarifa bungeni kuhusu mipango yake ya kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, na  kama ataiondoa nchi yake bila ya mkataba ifikapo Oktoba 31.

Waziri mkuu huyo mpya ameliambia baraza lake jipya la mawaziri kwamba Uingereza imo katika kipindi nyeti kabisa cha historia ya nchi hiyo. Bwana Johnson kwa mara nyingine amesisitiza azma ya kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya itakapofika tarehe 31 mwezi Oktoba au hata kabla ya hapo.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kukabiliwa na maswali magumu atakapolihutubia bunge baadae  leo. Mwanasiasa huyo amebakiwa na siku100 ili kuweza kuitimiza ahadi ya kuutekeleza mchakato wa Brexit, baada ya kusema kuwa serikali ya waziri mkuu wa hapo awali ilipoteza muda wa miaka mitatu kutokana na  kutojiamini katika suala la Brexit.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: picture-alliance/empics/B. Lawless

Kwa upande wake kiongozi wa Ireland Leo Varadkar amesema wazo kwamba Waziri Mkuu mpya Boris  Johnson ataweza kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya juu ya kufikia mkataba mpya wa Brexit, haliakisi hali ya ukweli.

Naye kiongozi wa chama cha Democratic  Unionist  Party, DUP Arlene Forster amesema matokeo ya kura  ya maoni juu ya Brexit yanapaswa kutekelezwa.

Wakati huo huo kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amemtaka Waziri  Mkuu mpya Boris Johson akubali kuitisha uchaguzi utakaompa uhalali wa kuongoza nchi. Lakini bwana Johnson ameashiria kwamba haoni ulazima wa kuitisha uchaguzi kabla ya kuutekeleza mchakato wa Brexit, yaani kuiondoa Uingereza Umoja  wa  Ulaya.

Katika baraza jipya la mawaziri bwana Johnson amewateua watu aliowahi kufanya nao kazi ikiwa pamoja na Waziri mpya wa  mambo ya nje Domic Raab, Waziri wa fedha Sajid Javid, Waziri wa Mambo ya Ndani Priti Patel na mnadhimu wa chama cha Kihafidhina bungeni Jacob Rees-Mog.

Vyanzo:/DPA,AFP,APE/https://p.dw.com/p/3MgOJ

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW