Boris Johnson ahangaikia mafuta Ghuba
16 Machi 2022Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson yuko ziarani eneo la Ghuba na kwenye ziara hiyo akiwa AbuDhabi amesisitiza haja ya kufanya kazi pamoja kuleta utulivu katika masoko ya nishati dunia.
Waziri mkuu Boris Johnson katika mazungumzo yake na kiongozi wa Umoja wa Falme za kiarabu,mrithi wa ufalme Mohammed bin Zayed al-Nahayan yaliyofanyika leo amesisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano ili kutuliza hali kwenye soko la mafuta duniani.
Boris Johnson alikutana na mwanamfalme huyo katika kituo chake cha kwanza cha ziara yake eneo la Ghuba ambayo ni sehemu ya juhudi za kutafuta washirika zaidi wa kusambaza mafuta pamoja na kuongeza mbinyo dhidi ya rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusu uvamizi wake nchini Ukraine.Aidha jioni hii waziri mkuu huyo wa Uingereza alifikia makubaliano ya kimkakati na Saudi Arabia.
Uingereza kama zilivyo nchi nyingine nyingi za Magharibi inakabiliwa na tatizo la ongezeko la bei ya nishati na kwahivyo Johnson anataka kuwashawishi wazalishaji mafuta kuongeza viwango vya uzalishaji bidhaa hiyo pamoja na kutafuta wasambazaji wengine ili kujaribu kuwasaidia watumiaji kwenye nchi hizo na kupunguza utegemezi wa nishati inayosambazwa kutoka Urusi.
Kufikia sasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambazo mahusiano yao ya karibu na Marekani yanakabiliwa na mashaka,zimeipuuza miito ya Marekani ya kuzitaka ziongeze uzalishaji wa mafuta ili kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta ghafi ambayo inatishia kuitumbukiza dunia katika mporomoko wa kiuchumi baada ya Urusi kuivamia Ukraine.
Johnson amesema ulimwengu unapaswa kuondokana na utegemezi wa nishati ya Urusi na kumuachia Putin mafuta na gesi yake,akiongeza kusema kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za kiarabuni ni washirika muhimu wa kimataifa katika juhudi hizo.
Nchi hizo mbili za Ghuba ni miongoni mwa nchi chache za kundi la nchi zinazosafirisha mafuta duniani la OPEC ambazo zina uwezo wa akiba ya mafuta ya kuongeza uzalishaji na uwezekano wa kuziba pengo la usambazaji mafuta kutoka Urusi.Lakini nchi hizo zimeonesha kujaribu kujiweka katika nafasi ya kutoegemea upande kati ya washirika wake wa kambi ya Magharibi na Moscow ambaye ni mshirika wao katika kundi linalojulikana kama OPEC+.
Kundi hilo limekuwa likiongeza uzalishaji hatua kwa hatua kila mwezi kwa kutoa mapipa 400,000 kwa siku,na kuonesha kukataa shinikizo la kuwataka waongeze uzalishaji haraka.Kabla ya mkutano na Boris Johnson, Duru zilishasema, Umoja wa Falme za kiarabu bado umebaki na msimamo uliokubaliwa na kundi la OPEC+
Nchi hiyo tajiri ya Ghuba imeimarisha uhusiano wake na Moscow pamoja na Beijing katika kipindi cha miaka michache iliyopita na hata mwezi uliopita ilijizuia kuupigia kura muswaada wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Katika mkutano wake na mrithi wa ufalme, Mohammed bin Zayed al-Nahayan,wamekubaliana pia kuhusu haja ya kuimarisha usalama,ulinzi na ushirikiano wa kiintelijensia kukabiliana na vitisho ikiwemo kutoka kwa wahouthi ambao wamekuwa wakiendeleza mapambano nchini Yemen dhidi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo