1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson akabiliwa na mbinyo kuhusu "Partygate"

26 Januari 2022

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anajiandaa kwa matokeo ya uchunguzi wa sherehe zilizofanyika katika makao na afisi yake ya Downing Street wakati nchi hiyo ilikuwa chini ya vizuizi vya corona

London | Premierminister Boris Johnson
Picha: Rob Pinney/Getty Images

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameitetea leo rekodi ya utendaji wa serikali yake na kuapa kuendelea kupambana wakati akijiandaa kwa ripoti inayoweza kuwa na madhara makubwa ambayo ilichunguza sherehe zilizoandaliwa ofisini mwake wakati wa vizuizi vya maambukizi ya corona.

Soma pia: Boris Johnson: Shujaa wa Brexit chini ya shinikizo la 'partygate'

Ripoti ya mwisho kutoka kwa uchunguzi uliofanywa na mtumishi wa umma mwandamizi Sue Gray inatarajiwa kuwasilishwa kwa serikali baadae leo au kesho. Uthibitisho kuwa jeshi la polisi ya London sasa limeanzisha uchunguzi wake kuhusu sakata hilo pia huenda ukatatiza kuzinduliwa kwa ripoti hiyo ya Gray, lakini vyama vya upinzani vinasisitiza kuwa lazima ichapishwe kwa ukamilifu.

Johnson, katika kikao cha kila wiki cha kujibu maswali bungeni kilichojaa hisia kali, amesema asingetaka kuzungumzia zaidi matokeo ya kashfa hiyo iliyopewa jina la Partygate, wakati kukisubiriwa uchunguzi.

Polisi ya London inachunguza pia kashfa ya "Partygate"Picha: Aaron Chown/empics/picture alliance

Lakini alisema serikali – kuanza jinsi ilivyoshughulikia janga la corona hadi kuufufua uchumi, na kuzileta nchi za Magharibi pamoja dhidi ya vitisho vya Urusi kwa Ukraine – haiendi kokote. "Nataka tu kuongeza kwamba tumechukua maamuzi magumu, tumefanikiwa katika kufanya maamuzi makubwa, na tunaendelea, hasa mimi ninaendelea na kazi."

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Keir Starmer anatarajia kuwa ripoti hiyo itatolewa wakati wowote sasa na kuwa Johnson atatoa jibu lake

"Chochote atakachosema katika taarifa yake baadaye leo au kesho hakitabadilisha ukweli, si huyu ni Waziri Mkuu na serikali ambayo haijaonyesha lolote ila kuudharau ustaarabu, uaminifu na heshima ya nchi hii?"

Soma pia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikaidi wito wa kujiuzulu

Gray, anayelezewa kuwa mtekelezaji hatari wa haki serikalini, amekuwa akichunguza ufichuzi kuwa wafanyakazi wa ofisi ya waziri mkuu walifanya sherehe za mara kwa mara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita wakati nchi ilikuwa chini ya vizuizi vikali vya corona.

Johnson, amekabiliwa na dhahabu ya umma kuhusiana na sherehe hizo. Waziri mkuu huyo alihudhuria hafla kadhaa, ukiwemo mkusanyiko wa watu wengi ulioandaliwa kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa Juni 2020 katika wakati ambao watu hawakuruhusiwa kujumuika pamoja.

Wengi kwenye mitandao ya kijami wameeleza jinsi walishindwa kuhudhuria matukio muhimu ya Maisha kwa kuheshimu sheria za kuzuia mikusanyiko, na hawakuweza kuwafariji wagonjwa na kujumuika na wenzao kuwaomboleza waliofariki kutokana na COVID.

afp