Boris Johnson akataa kujiuzulu
6 Julai 2022Katika kipindi cha saa 24 zilizopita waziri mkuu huyo ameshuhudia akikimbiwa na wimbi kubwa la watendaji wake serikalini ikiwemo mawaziri wake muhimu.
Ndani ya muda mfupi Boris Johnson amekimbiwa na washirika wake chungunzima serikalini.
Mbele ya bunge leo waziri mkuu Boris Johnson ameshikilia kwamba hakubaliani na wabunge kutoka chama chake wanaomtaka ajiuuzulu na kuweka mbele maslahi ya taifa.
Boris Johnson anasema haamini ni kinyume na maslahi ya taifa kuendelea kuweko kwake madarakani bali anaamini huu hasa ni wakati ambapo anatakiwa kusimama imara katika kuiongoza nchi.
soma pia: Mawaziri 2 muhimu wajiuzulu Uingereza, shinikizo kwa Johnson
ameliambia bunge kwamba wakati nchi inakabiliwa na shinikizo kuhusu hali ya kiuchumi,vita vikubwa kabisa ulaya tangu miaka 80 iliyopita ameitaja huu hasa ndio wakati ambao serikali inatarajiwa kuendelee kufanya kazi yake kikamilifu.
"Isifunge virago na kuondoka badala yake kuendelea na kazi na kutazama vitu ambavyo vina umuhimu zaidi kwa watu wa nchi hii'' Alisema Boris
Watendaji wake waendelea kujiuzulu
Watendaji wake 13 serikali ikiwemo mawaziri muhimu wa fedha na afya wamejiuzulu, maafisa hao wamejiuzulu wakisema hawezi tena kufanya kazi chini ya uongozi ulioandamwa na kashfa.
Kwa mara nyingine Dadiv Davis mbunge kutoka chama chake cha Conservative ambaye aliwahi kumtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu ameliambia bunge leo kwamba kwa mara nyingine anamuomba kiongozi huyo achukue hatua hiyo ya kiungwana ya kujiuzulu kutanguliza mbele maslahi ya nchi kabla ya maslahi yake binafsi.
Hivi sasa unaweza kusema kwamba waziri mkuu huyo wa Uingereza hivi sasa anapambania uhai wake wa kisiasa kufuatia kishindo hiki cha kujiuzulu watendaji wake na kashfa zinazomuandama.
Hata aliyekuwa mjumbe wake katika mazungumzo ya Brexit David Frost naye pia amejiunga na kundi linalomtaka ajiuzulu mara moja la chama chake cha wahafidhina.
soma pia:Boris Johnson aponea kura ya kutokuwa na imani naye
Lakini pia wako mawaziri wengine chungunzima waliomtetea waziri mkuu akiwemo naibu waziri mkuu Dominic Raab,waziri wa mambo ya nje Liz Truss na waziri wa mambo ya ndani Priti Patel.
Kujiuzulu kwa watendaji ni shinikizo lingine kwa Johnson
Mpaka hivi sasa kuendelea kuwa watiifu kwa Johson mawaziri hao kunaondowa uwezekano wa kuitishwa mara moja uchaguzi wa mapema nchini Uingereza.
Ili hicho kitoke ni mpaka atakapokubali Johnson kujiuzulu au kukabiliwa tena na kura ya kutokuwa na imani nae.
Kujiuzlu kwa watendaji muhimu na maafisa wa serikali ya Uingereza kumechochea na hatua ya kuteuliwa mnadhimu wa shughuli za serikali Chris Pincher ambaye wiki iliyopita aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kutuhumiwa kulewa na kufanya kitendo cha utovu wa nidhamu dhidi ya wanaume wawili.
Lakini ikidaiwa kwamba sio mara ya kwanza kwa afisa huyo kufanya vitendo vya ukosefu wa nidhamu.