Boris Johnson amuwashia moto Theresa May
2 Oktoba 2018Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya waziri mkuu Theresa May nchini Uingereza.Boris Johnson amesema mipango ya kujitoa Umoja wa Ulaya -Brexit ya waziri mkuu huyo inadharau katiba na kwamba itaidhalilisha Uingereza.Boris Johnson ameyasema hayo katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Conservative, mjini Birmigham.
Akizungumza katika mkutano huo wa chama Johnson amesema kukuubalia mpango ya waziri mkuu May kutamaanisha kwamba shughuli za kibiashara na viwanda za Uingereza pamoja na uchumi wa nchi hiyo kwa ujumla wake yatalazimika kufuata kanuni na sheria za Umoja wa Ulaya.
''Itamaanisha biashara za Uingereza na viwanda pamoja na uchumi wake kwa ujumla utalazimika kufuata sheria ambazo huenda zimetengenezwa kwa makusudi na Umoja wa Ulaya kuzuia ushindani wa kigeni na itamaanisha kwamba kila upuuzi uliopitishwa na Brussels kwa siku za baadae tutalazimika kuutekeleza na hatutokuwa na uwezo wala mamlaka ya kubadili wala kupinga.Na huo sio mwafaka badala yake hilo ni jambo hatari na sio salama sio kwa uchumi wetu wala kisiasa.Wanachama wenzangu hii sio demokrasia,hicho sicho tulichokipigia kura.''
Mpinzani huyo mkuu wa mpango wa bibi May wa Brexit anasema kinachopendekezwa na waziri mkuu huyo ni hatari na kitaiweka Uingereza katika hali isiyokuwa salama kisiasa na kiuchumi. Johnson anataka kumuunga mkono May kwa kumlazimisha abadili mwelekeo wake wa sasa wa kutaka kujaribu kuubakisha uhusiano wa karibu wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya pindi Uingereza itajitowa katika Umoja huo mwezi Machi mwakani.
Na kwa mtazamo huo amewaasa wanachama wengine wa chama hicho cha Conservative kutafakari kwa makini akisema kwamba kinachopendekezwa sicho walichokipigia kura na wala sio demokrasia.Boris Johnson na mwanaharakati mkubwa anayepigia debe Uingereza kujitowa katika Umoja wa Ulaya lakini anamashaka makubwa juu ya kile kinachopendekezwa na Theresa May katika suala hilo anaamini kwamba chama cha Conservative kimepoteza imani yake na ametowa mwito kwa chama hicho kulisimamia suala la soko huru ili kutoupa nafasi upinzani unaongozwa na chama cha Labour kuingia madarakani.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha Ireland Kaskazini cha Democratic Unionist DUP Arlene Forster anasema hawezi kukubali kanuni mpya katika jimbo hilo ambayo ni tafauti na maeneo mengine ya Uingereza kama nchi kwa ujumla baada ya Brexit. Lakini Foster anahoji ni kwanini Umoja wa Ulaya uko tayari kukubali suluhisho la kiufundi ambalo linaweza kufanya kati katika eneo la bahari la Ireland lakini sheria hiyo hiyo haiwezi kufanya kazi katika eneo la mpaka wa nchi kavu wa Ireland.
Kuna uvumi kwamba Uingereza huenda ikaridhia sheria ya ukaguzi katika bandari za eneo la bahari ya Ireland kama sehemu ya mpango wa Brexit. Ikumbukwe kwamba suala linalosababisha mvutano kati ya bibi May na Umoja wa Ulaya hapa ni kuhusu jinsi ya kuepuka kuwepo mpaka kati ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland. Kadhalika katika mkutano wa Birmingham suala la uongozi wa chama cha Conservative pia linasikika kwenye kauli za wanasiasa wa chama cha Conservative.Mbunge Jacob Rees ambaye anaunga mkono mpango wa Brexit anasema kwamba pamoja na kwamba haiungi mkono sera ya waziri mkuu May ya Brexit bado anamuunga mkono katika uongozi wake na anataraji kwamba Theresa May atabadili mawazo yake juu ya sera yake inayopingwa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman