1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson aongoza mchujo kutafuta mwenyekiti wa Conservative

Daniel Gakuba
13 Juni 2019

Waziri wa zamani wa mambo ya nje nchini Uingereza Boris Johnson ameongoza duru ya kwanza ya mchujo wa wagombea wanaowania kuchukua uongozi wa chama cha Conservative kilicho madarakani nchini humo.

Großbritannien London | Boris Johnson
Boris Johnson, ameongoza katika mchujo wa kwanza wa kutafuta mwenyekiti mpya wa chama cha Conservative, UingerezaPicha: Reuters/H. Nicholls

Boris Johnson, mmojawapo wa vinara wa kampeni ya kuiondoa Uingereza katika umoja wa Ulaya amewaacha mbali kabisa wagombea wengine 9, akipata kura 114 kati ya 313 zilizopigwa na wabunge wa chama chake cha Conservative. Aliyekuja katika nafasi ya pili, Jeremy Hunt ambaye ni waziri wa sasa wa mambo ya nje, ameambulia kura 43, naye waziri wa mazingira Michael Gove akachukuwa nafasi ya tatu na kura 37.

Soma zaidi: Uingereza: Kinyang'anyiro cha kumrithi Theresa May chaanza

Wengine waliofanikiwa kuingia katika duru ya pili ya mchujo ni waziri wa mambo ya ndani Sajid Javid, aliyekuwa waziri ahusikaye na mchakato wa Brexit Dominic Raab, waziri wa afya Matt Hancock na waziri wa maendeleo ya kimataifa, Rory Stewart.

Mawaziri Jeremy Hunt na Michael Gove wanasemekana kugawana sawa kura za wabunge wenye msimamo laini kuhusu mchakato wa Uingereza kuondoka ndani ya Umoja wa Ulaya.

Tofauti kuhusu mtindo wa Brexit

Theresa May, alijiuzulu uongozi wa Conservative mwanzoni mwa JuniPicha: picture-alliance/AP/V. Mayo

Hunt na Gove wanapendelea nchi yao kupata makubaliano na Umoja wa Ulaya kabla ya kuondoka, tofauti na Johnson ambaye anataka Uingereza ifungashe vyake mwishoni mwa mwezi Oktoba, bila kujali kama itakuwa imefikia mwafaka na Umoja wa Ulaya au la. Sajid Javid amesema Uingereza kuondoka ndani ya Umoja wa Ulaya sio kigezo pekee cha Brexit.

''Tunapaswa kufahamu kwamba hatutatimiza matakwa ya waliopiga kura kuunga mkono Brexit, kwa kuondoka ndani ya Umoja wa Ulaya tu. Kura ya kuondoka huko haikuukosoa tu umoja huo, bali pia mfumo wa uongozi wa Uingereza, ambao wanaamini hauendi sawa tena, na dunia ambayo haina mustakabali mwema kwao.'' Amesema Javid.

Watatu waanguka katika mchujo wa kwanza

Wagombea 10 walikuwa wamejitosa katika kinyang'anyiro hichoPicha: picture-alliance/empics

Wagombea watatu wameng'olewa katika kinyang'anyiro hicho cha uongozi wa chama cha Conservative, ulioachwa na waziri mkuu wa sasa Theresa May alipojiuzulu mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni. Hao ni Mark Harper, Esther McVey na Andrea Leadsom ambao hawakuweza kupata kura 17, kiwango cha chini kinachohitajika ili mgombea aingine katika duru inayofuata.

Soma zaidi: Ulaya imepokea vipi kujiuzulu kwa May?

Kura ya pili ya mchujo itapigwa pia na wabunge wa Conservative  Jumanne ijayo, na Johnson anayehitaji kura 105 kusonga mbele katika duru ya mwisho anatumaini kuwa waliomuunga mkono leo wataendelea kusimama pamoja naye katika duru hiyo. Wagombea wawili wa mwisho watapigiwa kura na wanachama wote wa chama cha Conservative, na mshindi atakuwa mwenyekiti wa chama, na baadaye waziri mkuu.

Jana, bunge hilo la mjini London liliuangusha muswada uliowasilishwa na chama cha upinzani cha Labour, ukitaka bunge litenge siku moja baadaye mwezi huu, kupitisha sheria ya kuizuia Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya bila kupata makubaliano na Umoja wa Ulaya kuhusu uhusiano wao wa baadaye.

ape,afpe

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW