Boris Johnson aponea kura ya kutokuwa na imani naye
7 Juni 2022Uasi katika chama chake juu ya kashfa ya "partygate", unaonekana kuwa pigo kwa mamlaka yake na kumwacha Waziri Mkuu huyo katika hali ngumu ya kutafuta uungwaji mkono upya.
Johnson ambaye alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2019, amekuwa chini ya shinikizo kubwa baada ya kuandaa sherehe ya unywaji pombe katika ofisi yake ya Downing Street na makaazi yake wakati Uingereza ilipokuwa chini ya vizuizi vikali vya Corona.
Katika siku za hivi karibuni, Johnson alizomewa na umma wakati wa hafla za kusherehekea maadhimisho ya miaka 70 ya uongozi wa Malkia Elizabeth inayojulikana kama Jubilee ya Platinum.
Soma pia:Boris Johnson ziarani Belfast kuhusu mzozo wa Brexit
Wabunge kadhaa wamesema kura hiyo ya kutokuwa na imani na Johnson, ambapo wabunge 211 walipiga kura ya kumuunga mkono huku wabunge 148 wakipiga kura ya kutaka kumng'atua madarakani, licha ya kunusurika japo ilichora taswira mbaya tofauti na ilivyotarajiwa kwa Waziri Mkuu ambaye alionekana kuwa na ushawishi mkubwa bungeni baada ya kupata wingi wa viti bungeni katika historia ya Uingereza kwa zaidi ya miongo mitatu.
Ni mapema mno kutabiri kitakachotokea baada ya kura ya leo
Waziri wa zamani David Jones ameliambia shirika la habari la Reuters, "Boris Johnson atapata nafasi ya kupumua baada ya kura ya leo lakini pia anafaa kuelewa kipaumbele kinachofuata ni kujenga upya mshikamano wa chama."
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wameonyesha matumaini madogo kwa uongozi wa Johnson, mbunge mmoja wa chama cha kihafidhina ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema,"Ni wazi kuwa matokeo ya kura ya leo ni mabaya tofauti na ilivyotarajiwa na wengi. Ni mapema mno kusema kitakachotokea baada ya hapa."
Kwa kuponea kura ya kutokuwa na imani naye, Johnson amepata nafasi ya kupumua kwa angalau miezi mengine 12.
Soma pia: Boris Johnson ahangaikia mafuta Ghuba
Hata hivo, mtangulizi wake Theresa May licha ya kupata kura nyingi zaidi tofauti na Johnson wakati wa kura ya kutokuwa na imani naye mnamo mwaka 2018, alijiuzulu wadhfa wake miezi sita baadaye.
Baada ya kura hiyo bungeni, Waziri Mkuu huyo amesema hana nia ya kuandaa uchaguzi wa kitaifa licha ya baadhi kupendekeza afanye hivyo ili kurejesha mamlaka yake.
Amewaambia waandishi habari kuwa matokeo ya kura hiyo ni imara na ya kuyaridisha, akimaanisha kwamba serikali inaweza kushughulikia mambo mengine muhimu.
Licha ya ushindi wake, wabunge kadhaa wa chama cha kihafidhina wameelezea wasiwasi wao juu ya iwapo Johnson mwenye umri wa 57 amepoteza mamlaka ya kuitawala Uingereza, ambayo inakabiliwa na hatari ya kuporomoka kiuchumi na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.
Hata hivyo, baraza lake la mawaziri limejitetea kwa kufafanua mafanikio waliyoyapata serikalini ikiwemo utoaji haraka wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa ugonjwa wa UVIKO-19, na mwitikio mzuri wa Uingereza kwa mzozo wa Ukraine.