1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Pistorius ndiye waziri mpya wa ulinzi Ujerumani

17 Januari 2023

Pistorius alikuwa waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Lower Saxony na sasa anachukuwa nafasi iliyoachwa na Lambrecht aliyejiuzulu

Deutschland neuer Verteidigungsminister Boris Pistorius
Picha: Julian Stratenschulte/dpa/picture-alliance

Kansela Olaf Scholz amemteuwa  Boris Pistorius kuwa waziri wake mpya wa Ulinzi baada ya kujiuzulu jana Christine Lambrecht. Boris Pistorius hakuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitajwa katika orodha ya waliokuwa wakipendekezwa kuchukuwa nafasi hiyo iliyoachwa na Christine Lambrecht kutoka chama cha SPD aliyejiuzulu.

Ulimwengu wake tangu mwaka 2013 ulikuwa ni ule unahusiana na masuala ya kipolisi,usalama wa mambo ya ndani ,uhalifu wa kimtandao,uhamiaji  na michezo.

Soma pia: Waziri wa Ulinzi nchini Ujerumani ajiiuzulu.

Alikuwa ni waziri wa mambo ya ndani katika jimbo la Lower Saxony. Mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 62 sio tu anauzoefu wa muda mrefu wa kusimamia wizara bali pia ana vigezo vingine ambavyo hapana shaka vinahitajika katika wizara ya ulinzi ya shirikisho.

Picha: Sina Schuldt/dpa/picture alliance

Akizungumzia namna alivyopokea uteuzi wake mwanaisasa huyo alionesha kufurahishwa na uteuzi huo akisema

kwake  ni heshima kubwa kupewa wizara hii akifahamu pia umuhimu wa wizara hiyo na hasa katika kipindi hiki.''

Ni mtu anayejiamini na vile vile mpambanaji asiyekubali kushindwa. Sifa hizi hasa ndizo zinazohitajika kwenye wizara hiyo haraka kulirudisha jeshi la Ujerumani kwenye hadhi na  nafasi yake.

Baada ya Urusi kuivamia Ukraine Kansela Olaf Scholz aliahidi kutowa fedha kwa jeshi la Ujerumani dola bilioni 100, fedha hizo zikikusudiwa kuingia kwenye mfuko maalum utakaosimamia mikakati ya kuliboresha jeshi hilo kuwa la kisasa.

Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Jeshi la Ujerumani linalalamikia kukabiliwa na matatizo mengi kuanzia suala la kuwa na vifaa vya zamani, upungufu wa silaha na hata matatizo yao binafsi.

Kamishna wa bunge la shirikisho anayehusika na masuala ya jeshi la Ujerumani, Eva Högl, hivi karibuni alitowa  sura iliyoonesha namna hali ya jeshi la Ujerumani ilivyo mbaya  na kusema kwamba kwahakika kiwango cha fedha kinachohitajika kuruweka sawa mustakabali wa jeshi hilo ni yuro bilioni 300.

Pitorius ataapishwa alhamisi bungeni na mara tu baada ya hapo atakuwa na mkutano muhimu,na waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na ijumaa atakutana na mawaziri wa jumuiya ya kujihami ya NATO katika kambi ya jeshi la Marekani ya Ramstein watakaojadili juu ya kuipelekea msaada wa ziada Ukraine.

Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef