1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Bashar al-Assad hauko tayari kwa mabadiliko

10 Machi 2021

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema Utawala wa rais wa Syria Bashar al-Assad unazuia mjadala wowote wa kweli na hautaki uchaguzi huru na wa haki

Josep Borrell
Picha: Johanna Geron/AP Photo/picture alliance

Wakati wa kikao cha Bunge la Ulaya kuhusu Syria, Borrell alisisitiza kuwa Assad hataki mabadiliko na badala yake mnamo Juni mwaka huu, ataandaa uchaguzi wake mwenyewe kuhakikisha anashinda. Borrell amesema hakutakuwa na mwisho wa vikwazo, uhusiano wa kawaida ama msaada wa kujenga upya taifa hilo la Syria hadi kutakapokuwa na mabadiliko ya kisiasa.

Borrell ameongeza kusema kuwa ni miaka 10 sasa ya mikasa kwa watu wa Syria. Kuhama makazi yao, umaskini, uharibifu, mateso, kupotezwa,  mabomu ya mapipa na silaha za kemikali na kwamba walifikiri hawatahitajika kuona hali hiyo tena machoni mwao. Ameongeza kuwa nchi tano zina wanajeshi nchini Syria wakati huu na kwamba hata kwa msaada wa kijeshi wa Urusi na Iran,Assadhawezi kushinda na suluhisho la kisiasa pekee ndilo linaloweza kudumu.

Mnamo Machi 1 Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa tume yake ya uchunguzi kuhusu taifa hilo la kiarabu la Syria, ilisema kuwa baada ya muongo mmoja wa mapigano, maelfu ya raia waliowekwa kizuizini kiholela bado hawajulikani walipo huku maelfu ya watu wengine wakiteswa na kunyanyaswa kingono ama kufariki wakiwa kizuizini.

Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa/SANA

Mnamo Februari 25, Mkuu wa Masuala ya Kibinaadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock aliliambia baraza la usalama la Umoja huo kwamba takriban asilimia 60 ya raia wa Syria hawana uwezo wa kawaida wa kupata chakula salama na cha kutosha huku watu milioni 4.5 zaidi wakiingia katika orodha hii katika muda wa mwaka uliopita na kuonya kuwa ongezeko hilo huenda likawa la kuhofisha lakini haliwezi kusemekana kuwa la kushangaza.

Mwaka huu unaadhimisha muongo mmoja wa mzozo unaoendelea nchini Syria. Mzozo huo unasemekana kuwa mbaya zaidi wa kibinadamu kwa kizazi cha sasa ambao umesababisha watu wengi kupoteza makazi nchini humo na kuwa wakimbizi katika mataifa jirani. Kulingana na takwimu mpya za kitaifa kutoka kwa mpango wa chakula duniani WFP zilizochapishwa Februari 17 mwaka huu, takriban raia milioni 12.4 hii ikiwa karibu asilimia 60 ya idadi kamili ya watu nchini humo, kwasasa hawana chakula cha kutosha.

Mnamo mwezi Machi mwaka 2011, waandamanaji nchini humo walifanya maandamano ya kutaka kuhitimishwa kwa uongozi wa Assad ambao umekuwa mamlakani tangu babake Assad Hafiz al-Assad alipokuwa rais mwaka 1971. Serikali ya Syria chini ya uongozi wa rais Bashar al-Assad ulikandamiza maandamano hayo kwa kutumia polisi na vikosi vya kijeshi.

 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW