1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borrell ataka kusitishwa mazungumzo ya kisiasa na Israel

18 Novemba 2024

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amethibitisha kuwa hii leo atapendekeza juu ya kusitishwa mazungumzo ya kisiasa na Israel kuhusu vita vyake katika Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mnamo Oktoba 30, 2024
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Virginia Mayo/AP/dpa/picture alliance

Kabla ya mkutano huo wa Brussels, Borrell amesema kuwa watu wengi walijaribu kusitisha vita katika ukanda wa Gaza lakini hilo bado halijatokea na kwamba hakuna matumaini ya kufanyika.

Akiwahutubia wanahabari, Borrell amesema hiyo ndio sababu wanapaswa kuweka shinikizo kwa serikali ya Israeli, na pia kwa upande wa kundi la wanamgambo la Hamas.

Bidhaa kutoka maeneo ya Israel, zapendekezwa  kupigwa marufuku

Borrell pia anataka uagizaji wa bidhaa kutoka kwa makazi yanayokaliwa kimabavu na Israel katika ardhi za Palestina, ambayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, kupigwa marufuku.

Borrell ataka EU isimamishe mazungumzo ya kisiasa na Israel

Akizungumzia hatua hiyo inayotarajiwa kuchukuliwa na Borrell, waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi  Caspar Veldkamp, amesema leo kuwa Umoja huo wa Ulaya unahitaji kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na Israel wakati ambapo vurugu bado zinaendelea katika Mashariki ya Kati.

Mashambulizi ya Israel yawauwa watu katika maeneo mbali mbali

Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon, yamewauwa watu 11 katika eneo la kusini na sita mjini Beirut ikiwa ni pamoja na msemaji wa kundi la Hezbollah Mohammed Afif.

Shambulizi la Israel katika eneo la Beit Lahya kaskazini mwa GazaPicha: -/AFP

Siku ya Jumapili, shirika la ulinzi wa raia wa Gaza, lilisema kuwa watu 34 waliuawa wakiwajumuisha watoto huku mamia ya wengine hawajulikani walipo baada ya shambulizi la Israel kulenga jengo la makazi la gorofa tano mjini Beit Lahia.

Juhudi za uokoaji zaathirika kutokana na mashambulizi 

Msemaji wa shirika hilo Mahmud Bassal, ameliambia shirika la habari la reuters kwamba, uwezekano wa kuwaokoa majeruhi zaidi unapungua kwa sababu ya mashambuliziyanayoendelea .

Hata hivyo jeshi la Israel limesema kuwa kuna shughuli za kigaidi zinazoendelezwa katika eneo hilo la Beit Lahia na kwamba mashambulizi kadhaa yanaelekezwa katika maeneo ya wanamgambo katika eneo hilo.

Jeshi la Israel lasema maafisa wake wawili wameuawa

Jeshi hilo pia limetangaza vifo vya maafisa wake wawili wakati wa mapambano katika eneo la kaskazini mwa Gaza .

Katika mashambulizi mengine hatari, Bassal amesema watu 15 waliuawa katika eneo la katikati mwa Gaza na wengine watano katika mji wa kusini wa Rafah.

Mjumbe mkuu wa Marekani kufanya ziara nchini Lebanon

Mbali na hayo,  mshauri wa cheo cha juu wa rais wa Marekani Joe Biden, Amos Hochstein, anatarajiwa kufanya ziara nchini Lebanon kesho Jumanne, huku nchi hiyo ikitarajiwa kutoa majibu yake kuhusu pendekezo la Marekani la usitishaji wa mapigano.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW