1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borrell: Uaminifu kati ya Umoja wa Ulaya na China umepungua

13 Oktoba 2023

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell yuko ziarani nchini China ambako amefanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa zaidi duniani.

EU l Hoher Vertreter der Union für Außen- und Sicherheitspolitik, EU-Kommision - Josep Borrell
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell Picha: Frederick Florin/AFP via Getty Images

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameonya kwamba China ina kazi kubwa ya kufanya ili kurejesha imani ya wawekezaji wa nchi za Magharibi, na kwamba kukosekana kwa usawa wa kibiashara kumedhoofisha uaminifu kati ya China na jumuiya hiyo yenye jumla ya mataifa 27.

Borrell ameangazia tatizo la kukosekana kwa usawa wa kibiashara kati ya Umoja huo na China ambao unagharimu yuro bilioni 400 ambazo ni sawa (dola bilioni 423) na kusema hilo linahusu si tu idadi ya uzalishaji bali pia ubora wake.

Soma pia: Borell: Uamunifu kati ya Umoja wa Ulaya na China umepotea

Mwanadiplomasia huyo wa Umoja wa Ulaya amesema kumekuwepo na tatizo la kudumu kwa makampuni ya Ulaya wakati yanapojaribu kulifikia soko la China, huku akisisitiza kuwa ni kwa maslahi ya pande mbili kurekebisha hali hiyo ya kukosekana kwa usawa katika mahusiano ya kiuchumi na kibiashara.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell (kushoto) akisalimiana na Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi mjini Munich, Ujerumani(18.02.2023)Picha: Ren Pengfei/Xinhua/picture alliance

Borrell amesema ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa,  juhudi za Ulaya za kupunguza utegemezi wake kwa China zinaweza kuongeza kasi zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Aidha Borrell amebainisha wazi kuwa uaminifu kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na China 'umepungua':

"Kuaminiana ndio nguzo ya mahusiano yoyote ya kibinadamu, na tuafikiane kwamba uaminifu wetu sote umepungua. Tunapaswa kufanya kazi ili kujenga upya uaminifu huu. Hautarudi kimuujiza, lazima urejeshwe kwa kushughulikiwa."

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amesema amekuwa na mazungumzo ya "kina, ya wazi na ya kirafiki" na Borrell kuhusu masuala mbalimbali na wamefikia makubaliano muhimu.

Soma pia: Ujerumani na Ufaransa zapongeza uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuchunguza ruzuku zinazotolewa na China

Katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na Borrell huko Beijing, Wang amesema China inazingatia kwa dhati wasiwasi wa mataifa ya Ulaya kuhusu masuala ya kibiashara, na kwamba Beijing itaandaa mazingira bora ya biashara kwa makampuni ya Umoja huo nchini China. Yi amesema hakuna mgogoro wa maslahi na kuongeza kuwa China na EU ni washirika.

Mizozo ya sasa yajadiliwa pia

Bendera za China na Umoja wa Ulaya (EU)Picha: Dursun Aydemir/AA/picture-alliance

Viongozi hao wawili wamezungumzia pia migogoro inayoendelea kwa sasa duniani, hususan vita vinavyoendelea huko Gaza kati ya Israel na kundi la Hamas, pamoja na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Borrell ameitaka China kutumia ushawishi wake kwa Urusi ili ikomeshe vita hivyo na kuyafufua makubaliano ya usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi. Borrell ameongeza kuwa hadi sasa, hakukuwepo aina yoyote ya msaada wa kijeshi wa moja kwa moja uliotolewa na China kwa Urusi.

Kwa muda sasa,  Umoja wa Ulaya umekuwa na mvutano na China kuhusu masuala ya kiuchumi na kibiashara. Kwa sasa, sera ya Umoja huo wenye makao yake mjini Brussels, Ubelgiji ni kwamba China ni "mshindani wa kiuchumi na mpinzani wa kimfumo."

Lakini licha ya tofauti zao, pande hizo mbili zina nia ya kuanza tena mazungumzo kufuatia mtikisiko wa kiuchumi uliosababishwa na janga la UVIKO-19 na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Vyanzo: (AFP,RTR)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW