Borussia Dortmund bado ngangari katika Bundesliga
25 Februari 2019Katika ligi ya Ujerumani Bundesliga , viongozi wa ligi hiyo kwa sasa Borussia Dortmund wameendelea kung'ang'ania katika mbio zao za kuwania kutwaa taji la ligi ya Bundesliga msimu huu kwa ushindi wa mabao 3-2 jana Jumapili dhidi ya Bayer Leverkusen.
Ushindi huu wa Borussia Dortmund ni wa kwanza katika michezo minne ya ligi na kuiweka timu hiyo pointi tatu juu ya msimamo wa ligi ikiwatangulia mabingwa watetezi Bayern Munich, ambayo ilisogea hadi kuwa sawa kwa pointi na BVB baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Hertha Berlin siku ya Jumamosi.
Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa kati ya Bayern Munich na Hertha BSC Berlin siku ya Jumamosi , lakini Jacob Safari alifunga safari hadi katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund na alishuhudia pambano kati ya Borussia Dortmund ikipambana na Bayer 04 Leverkusen katika mchezo uliokuwa na mbinyo mkali kwa Dortmund wakati wakijua wazi kwamba kufungwa nyumbani kutavunja rekodi yao ya kutofungwa nyumbani katika mchezo wa ligi msimu huu, na pia watakuwa wamefikiwa kwa pointi na Bayern Munich.
RB Leipzig kucheza Jumatatu
Leverkusen ilikuwa imepata ushindi katika michezo yake minne iliyopita chini ya kocha wao mpya Peter Bosz, ambaye alitengana na BVB Desemba mwaka 2017, wakati kikosi chake kilikuwa katika kipindi chake cha muda mrefu bila ushindi.
RB Leipzig iliyoko katika nafasi ya 4 katika msimamo wa ligi inajimwaga dimbani leo Jumatatu kupambana na Hoffenheim ikiwa nyumbani. Lakini timu ambayo inashangaza kila mchambuzi wa kandanda kwa hivi sasa ni VFL Wolfsburg ambayo imeendelea kupata ushindi tena wa kishindo wiki baada ya wiki.
Na wiki hii ilipata ushindi dhidi ya timu iliyoko katika nafsi ya tatu Borussia Moenchengladbach wa mabao 3-0 ikiwa ugenini na kuchupa hadi nafasi ya 5 ikiwa na pointi 38.
Hata hivyo timu iliyofanya vibaya wiki hii ni Schalke 04 ambayo ilikubali kipigo cha mabao 3-0 mikononi mwa Mainz 05 na kubakia katika nafasi ya 13 na kuchungulia shimo la kushuka daraja. Kutokana na hali hiyo mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo Christian Heidel ameamua kuachia ngazi msimu huu ukimalizika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape /
Mhariri: Mohammed Khelef