Borussia Dortmund yaendelea kukaa kileleni
21 Januari 2019
Ligi ya Ujerumani Bundesliga, Borussia Dortmund imemaliza wiki ya kwanza ya Bundesliga katika mwaka huu 2019 ikiwa bado imeendelea kuweka mwanya wa pointi sita juu ya mabingwa watetezi Bayern Munich wakati mbio za kufukuzia ubingwa wa Ujerumani msimu huu ukiendelea kuleta msisimko mkubwa. Borussia Dortmund ilitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RB Leipzig siku ya Jumamosi kufuatia kipigo ilichotoa Bayern Munich cha mabao 3-1 dhidi ya Hoffenheim siku ya Ijumaa.
Leon Goretzka , ambaye alipachika mabao mawili katika ushindi wa Bayern dhidi ya Hoffenheim , mzaliwa wa mji wa Bochum alisema baada ya mchezo huo kuwa ushindi wa kwanza baada ya mapumziko ya majira ya baridi ni muhimu, kuendelea katika njia sahihi. Msako bado unaendelea kuisaka Dortmund, aliongeza.
Nico Schulz , ambaye alifunga bao pekee la Hoffenheim katika mchezo huo , alisema Kingsley Coman amemsamehe kwa kumfanyia faulo mbaya kabisa ambayo ilimuweka nje ya uwanja Mfaransa huyo kwa miezi mitatu. Kulikuwa na hali ya kupendeza wakati wachezaji hao wakikumbatiana wakati wa mapumziko siku ya Ijumaa wakati Schulz alipomkumbatia Coman na kuomba msamaha kwa rafu ile aliyofanya ambayo ilimuweka mchezaji huyo wa pembeni wa Bayern nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Eintracht Frankfurt inaelekea katika kufuzu kucheza katika Champions League msimu ujao, na wanaripotiwa kuwa na matumaini kwamba wanaweza kuendelea kuwa na washambuliaji wao watatu wanaotia fora katika kupachika mabao kwa timu hiyo msimu ujao. Mshambuliaji Luka Jovic akiwa ba mabao 13, Sebastian Haller mabao 10 na Ante Rebic mabao 6 wanatia fora katika ligi ya Ujerumani Bundesliga hivi sasa.
Jovic mwenye umri wa miaka 21, ambaye anaongoza ufungaji katika ligi hadi sasa, ana mkataba wa kuazimwa na Frankfurt wanasema wanataka kulipa euro milioni 6 ambazo Benfica inataka kupata saini ya mchezaji huyo Mcroatia mwenye umri wa miaka 21.
Frankfurt yachachamaa
Frankfurt iko katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 30, pointi moja nyuma ya timu iliyoko katika nafasi ya 4 , RB Leipzig yenye pointi 31. Frankfurt iliikandika Freiburg kwa mabao 3-1 siku ya Jumamosi.
Borussia Moenchengladbach iliendelea kujiimarisha katika nafasi ya tatu nyuma ya Bayern Munich kwa kuishinda Bayer 04 Leverkusen kwa bao 1-0, wakati VFL Wolfsburg ilishindwa kutamba mbele ya Schalke 04, pale ilipozabwa kwa mabao 2-1 ugenini na kushindwa kusogea na kukaribia nafasi ya kucheza katika Champions League.
Schalke sasa imechupa kutoka nafasi ya 14 na kutua katika nafasi ya 12 , ikiwa na pointi 21. Ikumbukwe kwamba Schalke bado imo katika eneo la hatari ya kushuka daraja kwani inapishana kwa pointi 6 tu na timu zilizoko katika eneo hilo.
Wakati huo huo Schalke 04 imemuondoa nahodha wake na mlinda mlango Ralf Fäemann kwa ajili ya pambano la Jumapili dhidi ya Wolfsburg , mwezi mmoja kabla ya pambano lake la Champions League katika awamu ya mtoano wa timu 16 dhidi ya Manchester City. Faemann mwenye umri wa miaka 30 , ambaye ameitumikia Schalke katika michezo 228 ya Bundesliga na ambaye alianzia kutoka utotoni katika klabu hiyo, nafasi yake ilichukuliwa na mlinda mlango wa timu ya taifa ya Ujerumani chini ya miaka 21 Alexander Nuebel katika mchezo wa kwanza wa klabu hiyo jana baada ya mapumziko ya majira ya baridi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre / ape
Mhariri: Josephat Charo