Borussia ina sura mbili tofauti katika Bundesliga na Champions League
3 Novemba 2014Penalti ya dakika za mwisho iliyowekwa wavuni na Arjen Robben imewapa mabingwa watetezi Bayern Munich na viongozi wa ligi ya Bundesliga msimu huu ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund matokeo yaliyoiweka timu hiyo pointi nne juu ya msimamo wa ligi na kuwaporomosha mahasimu wao katika zoni ya kushuka daraja ikiwa katika nafasi ya 17.
Hakuna anayefahamu kwa hakika nini kinaisibu Borussia Dortmund ambapo katika kinyang'anyiro cha Champions League inang'ara pamoja na kombe la shirikisho DFB Pokal , lakini katika Bundesliga hali haiko shwari kabisa. Dortmund imeangukia pua kwa mara ya tano mfululizo na ina pointi saba tu kutokana na michezo kumi ya Bundesliga.
Bayern Munich yang'ara katika der klassiker
Bayern Munich ina pointi 24 kutokana na michezo kumi, ikifuatiwa na VFL Wolfsburg, ambayo imeishindilia VFB Stuttgart kwa mabao 4-0 katika pambano lililiofanyika siku ya Jumamosi. Hata hivyo mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben mbali na Dortmund kuwa katika nafasi isoyostahili , lakini huo ulikuwa mchezo ambao ni muhimu sana kwao.
"Kila mtu anacheza ili kushinda . Huo ndio mchezo. Huu ni mchezo ambao sio tu ulikuwa muhimu kwa leo, lakini hata kwa wakati ujao ni muhimu. Dortmund ni timu ambayo inaweza kufika mbali katika Champions League . Ndio sababu ni lazima kutumia michezo kama hii, bila kujali ni kiasi gani timu iko katika msimamo wa ligi. Ndio sababu nimeridhika na jinsi tulivyocheza leo."
Makamu bingwa Borussia Dortmund imekuwa ikiyumba msimu huu na haijapata dawa ya kujitoa kutoka katika hali hiyo isiyoeleweka kama anavyosema mlinzi wa Dortmund Lukasz Piszczek.
"Tutajaribu tena .TZunapambana na tuna mchezo muhimu Jumanne. Baada ya hapo inakuja Borussia Moenchengladbach. Mchezo huo pia si rahisi.Kwa vyovyote vile tunapaswa kujitahidi."
Freiburg imepata ushindi wake wa kwanza katika Bundesliga jana baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mjini Kolon. Kwa kocha Christian Streich hilo ni jambo linalofurahisha sana.
"Ni jambo zuri sana. Timu imefanikiwa na imestahili kushinda. Imepambana vikali na imeonesha mchezo mzuri na imefanikiwa.Tumefanyakazi vizuri na kuupeleka vizuri mpira kwa adui . Tulikuwa na nidhamu ya hali ya juu.Tumefanikiwa . Tumeonesha ukomavu wa hali ya juu, na hii ni muhimu kwetu kwamba katika mchezo kama huo , tumeonesha hali hiyo ya ukomavu."
Paderborn yatanua misuli
Timu iliyopanda daraja msimu huu FC Paderborn imeendelea kuzitikisa timu zenye uzoefu katika ligi hiyo , ambapo jana imefanikiwa kuipiga mwereka timu ya muda mrefu katika Bundesliga Hertha Berlin kwa mabao 3-1 . Nini siri ya mafanikio ya timu hii inayotoka katika mji mdogo wa Paderborn. kocha wa timu hiyo Andre Breitenreiter anasema.
"Mafanikio yetu hayakutarajiwa, kila mmoja alikuwa akisema hii ni timu namba moja ya kushuka daraja na kutoka hapo tulianza kufanyakazi kwa juhudi zote, na kila mmoja wetu kujifunza zaidi. Inafurahisha kuangalia, vijana wakicheza mpira safi na wa kupendeza."
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / zr
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman