Borussia Moenchengladbach bado iko kileleni mwa Bundesliga
9 Desemba 2019
Ligi ya Ujerumani Bundesliga, imeendelea katika mchezo wake wa 14 na viongozi Borussia Moenchengladbach wamedhihirisha nia yao ya kutoroka na taji hilo msimu huu, baada ya kung'ang'ania kileleni mwa msimamo wa ligi, baada ya kuwapiga mweleka mabingwa watetezi Bayern Munich kwa mabao 2-1 nyumbani. Katika mchezo huo Bayern walifanya kila waliloweza kupata ushindi , baada ya kupapaswa tena katika mchezo uliopita dhidi ya Bayer Leverkusen wiki iliyopita, wakitaka kusahihisha mkosa yao. Lakini walijikuta wanagonga mwamba kwa kikosi cha kocha Marco Rose na kuangukia pua. Nini kilitokea huyu hapa kocha wa mpito wa bayern Hansi Flick:
"Bila shaka tuliudhibiti mchezo, tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga. Kwa bahati mbaya mwishowe hatukuweza kuuweka mpira wavuni. Na baada ya kuwa sare ya 1-1 Gladbach ilionesha , ni kwanini wako hapo walipo, kwani wanacheza kwa kushambulia. Kwasababu wana nguvu kubwa katika ushambuliaji. Na tulishindwa kuutawala mchezo, kama tulivyofnya katika kipindi cha kwanza. Hatujaridhishwa na hali hiyo, kwa kile ambacho tumekifanya katika michezo yote miwili bila kupata pointi."
Nae kocha wa Borussia Moenchengladbach Marco Rose anasema timu yake imepigana kiume hadi kuuangusha mbuyu.
"Na ningependa kuipongeza sana timu yangu. Hii inaonesha , kwanini tuko juu. Hatukudhibitiwa, badala yake tuliweza kucheza kwa nia ya kupata ushindi. Hadi dakika ya 90 tulijaribu, kile ambacho wiki na miezi iliyopita tulikionesha na mwishowe tulizawadiwa penalti."
Timu zilizofaidika na mchezo wa 14 wa Bundesliga , ni pamoja na Borussia Dortmund, baada ya kupata ushindi wa kibarua wiki iliyopita dhidi ya Hertha Berlin , siku ya Jumamosi ilionesha kuwa bado ina makali, baada ya kuirarua Fortuna Dusseldorf kwa mabao 5-0. Mchezaji wa kati wa Dortmund Julian Brandt anaelezea hisia zake baada ya muda mrefu kikosi hicho kutumbukia katika ukosoaji mkubwa kuhusu uchezaji wake.
"Kimsingi mtu alitambua, kwa mara nyingine kutokana na mchezo ule tulioonesha, ambapo tulidhibiti kila eneo, bila shaka mabao mengi yangepatikana. Hii inatokea katika mchezo wa mpira. Na pia unaona, kwamba mwishoni pia tulikuwa tunajisikia raha uwanjani."
Leverkusen ilipata ushindi mwingine dhidi ya Schalke wa mabao 2-1, Union Berlin ikajiimarisha kubakia katika daraja la kwanza kwa kuikandika FC Kolon kwa mabao 2-0 , RB Leipzig inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi baada ya kuishinda Hoffenheim kwa mabao 3-1. Kocha Julian Nagelsmann aliwakaribisha waajiri wake wa zamani , lakini hakutoa nafasi kwao kuondok na pointi.