Bosi wa AC Milan apinga kuanza kwa Coppa Italia
29 Mei 2020Rais wa klabu ya AC Milan, Paolo Scaroni amesema anapinga mpango wa kurejea tena kwa msimu wa michezo nchini Italia kwa kuanza na mechi za nusu fainali na fainali za kombe la Coppa Italia katika kipindi cha siku chache.
Msimu wa mechi za soka nchini Italia ulisimamishwa mnamo tarehe 9 mwezi Machi mwaka huu kufuatia kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona baada ya mechi za mkondo wa kwanza wa nusu fainali kuchezwa.
Waziri wa michezo nchini Italia, Vincenzo Spadafora alithibitisha siku ya Alhamis kuwa ligi ya Serie A huenda ikarejea tena tarehe 20 mwezi Juni na kuendeleza kwamba kombe la Coppa Italia linaweza kukamilika kabla ya mikondo ya pili, mechi ya Napoli dhidi ya Inter Milan na Juventus dhidi ya AC Milan, mnamo Juni 13 na fainali kupigwa siku tatu badae.
"Tunatambua thamani ya kuweza kutoa mechi zote za ubora baada ya miezi kadhaa ya kusimamishwa kwa mechi za soka," Scaroni aliliambia shirika la habari la ANSA.
"Lakini, kwa mtazamo wa michezo, tunaona kuwa ni muhimu tukabuni mechi mbili kwa siku tatu baada ya zaidi ya miezi mitatu ya mapumziko."
Gazeti la dello Sport lilinukuliwa kwa kusema kuwa Inter Milan na Juventus pia walikuwa wanapingana na mipango hiyo.
Marais wengine wawili wa kilabu walikaribisha uamuzi wa serikali wa kuanza tena msimu mpya.
"Ninauhakika kuwa kwa kuanza tena hatua hii, mpira wetu wa miguu utaweza kudumisha kiwango hicho cha hali ya juu ambacho kinatambulika kote ulimwenguni,"alisema Claudio Lotito Rais wa Lazio, ambaye timu yake inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Serie A, wakiwa nyuma ya alama moja dhidi ya vinara, bibi kizee wa Turin, Juventus.
Rais Urbano Cairo wa klabu cha Torino alisema alikuwa na wasiwasi juu ya kuendelea msimu lakini sasa wamekubaliana inapaswa kuendelea.
"Sikuwa nikifikiria tu kile kinachovutia kwangu lakini juu ya mtazamo wa jumla na afya ya wachezaji na umma. Ndio sababu nilikuwa na shaka," aliiambia ANSA.
"Sasa, tumeamua kuendelea tena na ni wazi niko hapa kufanya mambo kwa njia bora," alisema Cairo.
Chanzo:Reuters