1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Botswana yaathiriwa vibaya na kuporomoka kwa biashara ya almas

15 Septemba 2009

<p>Madhara ya kufilisika kwa benki kubwa ya mkopo ya Marekani ya Lehman Brothers kulikopelekea kuporomoka kwa uchumi wa dunia mwaka mmoja uliyopita yameiathiri sana sekta ya biashara ya almas nchini Botswana.</p>

Mbuga za wanyama moja ya sekta zinazoipatia fedha za kigeni BotswanaPicha: J. Sorges

Madhara ya kufilisika kwa benki kubwa ya mkopo ya Marekani ya Lehman Brothers kulikopelekea kuporomoka kwa uchumi wa dunia mwaka mmoja uliyopita yameiathiri sana sekta ya biashara ya almasi nchini Botswana.

Nyumba za wageni katika mji wa machimbo ya almasi uliyoko kiasi cha kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Gaborone, hazina wateja kama ilivyokuwa hapo kabla hii yote ni kuyumba kwa uchumi wa dunia.

 Botswana nchi ndogo iliyoko kusini mwa Afrika, inafahamika sana kwa utoaji wa madini ya almasi.Mauzo ya almasi yenye thamani ya kiasi cha dola billioni 3 kwa mwaka, yameifanya Botswana kuwa nchi yenye maendeleo.

Ikitumia maneno, ´´Almasi kwa Maendeleo,´´ ikiwa ni kujaribu kukwepa mtizamo mbaya wa madini hayo katika soko la biashara kutokana na almasi ilivyotumika kufadhili vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Afrika Magharibi, Botswana ilifanikiwa kuvuna mapato mengi ambayo yamechangia asilimia 40 ya pato lake.

Lakini hata hivyo nchi hiyo imeendelea kuongoza kuwa nchi yenye idadi kubwa ya wanawake watu wazima wasiyojua kusoma wala kuandika barani Afrika, na msukosuko huo wa uchumi duniani uliyosababishwa na kufilisika kwa benki ya kimarekani ya Lehman Brothers, umeathiri juhudi za kukabiliana na hali hiyo.

Gracious Oageng msichana mwenye umri wa miaka 19, ni miongoni mwa wasichana waliyoathrika na kuanguka kwa benki hiyo, kwani sasa ndoto yake ya kupata ufadhili wa masomo kutoka serikali imetoweka.

Mapato ya serikali yameshuka, kutokana na mauzo hafifu ya almasi katika soko la duniani ambako kumesababishwa na hali mbaya ya kuporomoka kwa uchumiwa dunia.

Binti huyo anasema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, lakini safari hii imesema kuwa hakuna fedha kwahiyo imepunguza idadi ya wanafunzi wanaopata ufadhili huo.

Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita wananchi wote wa Botswana ambao idadi yao haipindukii millioni 2, wameonja adha ya hali iliyoko mbele yao, yaani vipi maisha yatakavyokuwa bila ya mapato ya almasi.

Keith Jefferis ambaye ni mshauri wa masuala ya uchumi mjini Gaborone, anasema kuwa, katika kipindi hiki ambacho hakuna usafirishaji wowote wa almasi nje, ni funzo kwa hali itakavyokuwa wakati madini hayo ya almasi yatakapokuwa yamemalizika, na kwamba hilo ni somo zuri.

Maafisa wa serikali wanasema kuwa hifadhi ya almasi nchini Botswana itaanza kupungua mnamo kipindi cha miaka 10 ijayo.

Kampuni ya Debswana inayoshughulika na uchimbaji wa almasi nchini humo mwaka huu imepunguza robo ya gharama zake, ambapo imepunguza wafanyakazi 900 kati ya 6,200 iliyowaajiri.

Mbali ya hivyo, serikali ya nchi hiyo ambayo kwa miaka mingi bajeti yake imekuwa ikijitosheleza na kuwa na ziada ya fedha, imejikuta ikiingia katika madeni.

Mwezi Mei ililazimika kuomba mkopo wa dola millioni 825 kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha kufua umeme.Mwezi June ikawasilisha ombi Benki ya Mendeleo ya Afrika la kutaka mkopo wa dola billioni moja unusu ili kufidia nakisi katika bajeti yake.Kila sekta nchini humo imeathirika kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Katika mji mdogo wa Letlhakane ambako kuna mgodi wa almasi uliyoanza kufanya kazi miaka 35 iliyopita,wateja katika maduka na mabaa hawaonekani tena, wafanyakazi wa mgodi huo wanalalamika  kuwa mishahara yao imepunguzwa, na pia marupurupu mengine yamefutwa.

Mwandishi:Aboubakar Liongo/Reuters

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW