1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika kutogembea muhula mwingine wa urais

12 Machi 2019

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika ametangaza kwamba hatogombea urais kwa muhula wa tano kwa lengo la kumaliza maandamano ya wiki kadhaa kuipinga hatua yake hiyo.

Algerien | Abdelaziz Bouteflika
Picha: imago/photothek/T. Trutschel

 Katika barua yake iliyosomwa kupitia televisheni ya taifa, APS, Rais Bouteflika ameapa kwamba hatogombea tena uchaguzi wa urais, baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miaka 20. Aidha, Bouteflika ameahirisha uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliokuwa ufanyike Aprili 18 na anakusudia kufanya mageuzi kadhaa katika mfumo wa kisiasa na katiba nchini Algeria.

Bouteflika amesema ameufikia uamuzi huo ili kufanya marekebisho katika serikali yake haraka iwezekanavyo na kwamba mabadiliko hayo yanatokana na madai ya wananchi wa Algeria. Amebainisha kuwa ataunda jopo ambalo litapanga tarehe mpya ya uchaguzi wa urais.

Maelfu ya wananchi wa Algeria walijitokeza mitaani kushangilia uamuazi huo wa Bouteflika. Honi za magari zimekuwa zikisikika barabarani kwenye maeneo ya kati ya miji nchini humo, huku baadhi ya Waalgeria wakipepereusha bendera za taifa hilo. Taarifa zinaeleza kuwa polisi hawakuonekana mitaani wakati wa shamrashamra hizo.

Waalgeria wakifurahi baada ya tangazo la BouteflikaPicha: Reuters/Z. Bensemra

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita Algeria imekumbwa na maandamano ya kuipinga hatua ya Bouteflika, mwenye umri wa miaka 82, kugombea urais. Aidha, waandamanaji hao kwa muda mrefu wamelalamikia matatizo ya rushwa pamoja na sera mbaya za kiusalama.

Kiongozi huyo amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipougua kiharusi mwaka 2013, na alirejea Algeria Jumapili jioni baada ya kupatiwa matibabu yaliyosemekana kuwa ni ya kawaida mjini Geneva, Uswisi.

Waziri Mkuu ajiuzulu

Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri Mkuu wa Algeria, Ahmed Ouyahia ametangaza kujiuzulu wadhifa wake na rais amesema kuwa yatafanyika mabadiliko kadhaa katika baraza lake la mawaziri. Hata hivyo, nafasi ya Waziri Mkuu imezibwa na Noureddine Bedoui, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani. Bedoui amepewa jukumu la kuunda serikali mpya katika taifa hilo la Afrika ya Kaskazini.

Lakhdar Brahimi akizungumza na wanahabariPicha: picture-alliance/dpa/M. Messara

Bouteflika alikutana pia na mkuu wa majeshi wa Algeria, Luteni Jenerali Gaed Salah na mwanadiplomasia mkongwe, Lakhdar Brahimi ambaye anaheshimika sana nchini humo. Akizungumza baada ya kukutana na Bouteflika, Brahimi waziri wa zamani wa mambo ya nje na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, alisema sauti za watu zimesikika.

''Vijana walioingia mitaani kwenye miji yetu na vijiji, waliwajibika ipasavyo na wametoa taswira nzuri ya nchi yetu kote duniani. Tunapaswa kuubadilisha mzozo huu katika mchakato wa kujenga na kuheshimika,'' alisema Brahimi.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian ameupongeza uamuzi uliochukuliwa na Rais Bouteflika wa kutogombea urais. Le Drian amesema amefurahishwa na uamuzi wa Bouteflika ili kuzuia maandamano ya nchi nzima na juhudi zake za kuuangalia upya mfumo wa kisiasa nchini Algeria.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW