Bozize ataka kuunda serikali na waasi
31 Desemba 2012Pamoja na ahadi ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, Rais Bozize pia amesema kuwa hatagombea tena muhula mwingine wa utawala katika uchaguzi wa mwaka 2016. Kauli hiyo ya Bozize imetolewa baada ya mazungumzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Thomas Boni Yayi.
Boni Yayi, ambaye ni Rais wa Benin, amesema kuwa Bozize yuko tayari kushiriki mazungumzo ya amani baina ya serikali yake na waasi ambayo yameandaliwa na Umoja wa Afrika mjini Libreville, Gabon ambayo yatakamilisha nia yake hiyo ya kuunda serikali ya pamoja.
Waasi wafikiria ahadi ya Bozize
Kwa upande wao waasi wa Seleka ambao kwa sasa wako umbali wa kilometa 75 nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, wamesema kuwa wanalifikiria tangazo hilo la Bozize. Msemaji wa muungano wa Seleka Eric Massi amekiamba kituo cha televisheni cha France 24 kuwa kwanza watakaa mezani kuangalia yaliyomo kwenye ahadi hiyo.
Massi ameongeza kuwa wao haja yao ya msingi si madaraka bali ni kuwawezesha wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kupata maendeleo stahiki na kuweza kujitegemea kiuchumi.
Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari zinasema kuwa waasi huenda wakaingia mjini humo hii leo, ambako tayari amri ya kutotembea ovyo imetolewa.
Wasiwasi watanda Bangui
Maelfu ya wakaazi wa mji mkuu huo wameyakimbia makaazi yao wakihofia usalama wao. Waliosalia wamekusanya shehena za vyakula na maji majumbani mwao wakijiandaa endapo waasi wataingia mjini humo. Mitaa iko kimya kutokana na kutangazwa kwa hali ya hatari na matembezi ya usiku yamezuiwa.
Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka mjini Bangui, Sylvain Groulx, alikiambia kituo cha televisheni cha Aljazeera kuwa wasiwasi wao uko kwa watu waliokimbilia msituni baada ya kusikia milio ya risasi.
Harakati za wiki tatu za waasi hao kulekea mji mkuu wa Bangui zimezua taharuki miongoni mwa raia wa koloni hilo la zamani la Ufaransa. Nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa masikini zaidi duniani licha ya utajiri mkubwa wa madini ya Urani, almasi na dhahabu iliyonayo.
Hata hivyo bado haijafahamika kama fursa hiyo ya kuunda serikali ya pamoja iliyotolewa na Bozize itakuwa dawa sahihi ya mzozo huo ambao unatishia miaka kumi ya utawala wake. Waasi wa Seleka wanamtuhumu Rais Bozize kwa kukiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2007 ambapo wapiganaji waliokubali kuweka chini silaha zao walipaswa kulipwa.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail