BRAZIL KUCHEZA NUSUFINAL YA COPA AMERIKA NA URUGUAY-ARGERNTINA NA COLUMBIA-MASHINDANO YA UBINGWA RIADHA WA AFRIKA BRAZZAVILLE YAMALIZIKA
19 Julai 2004MICHEZO
COPA AMERIKA-BRAZIL YAITIMUA MEXICO 4-0 NA KUINGIA NUSU-FINALI NA URUGUAY
KOMBE LA ASIA:KOREA KUSINI YAPAMBANA LEO NA JORDAN-KUWEIT NA EMIRATES
MASHINDANO YA UBINGWA RIADHA YA AFRIKA YAMALIZIKA BRAZZAVILLE:
COPA AMERICA:Kombe la mataifa la Amerika kusini:
mabingwa wa dunia Brazil jana waliizaba Mexico mabao 4:0 na hivyo imeingia nusu finali ya kombe hili kati yake na mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia-Uruguay.Ikicheza na wachezaji 10 tu, uruguay iliizaba Paraguay 3-1.Paraguay hapo kabla iliilaza Brazil 2:1.Asdriano aliipatia Brazil mabao 2 na sasa kufanya orodha ya mabao yake kuwa 5 kwa timu ya taifa.
Katika nusu-finali ya pili, Argentina itakumbana na Columbia hapo kesho mjini Lima, Peru. Argentina iliitoa Peru-wenyeji kwa bao 1:0 hapo jumamosi.
Kuna kila uwezekano kwamba finali ya mwaka huu ya Copa Amerika itawakumbanisha majirani na mahasimu 2 wakubwa wa dimba huko Amerika Kusini:Brazil na Argentina. Finali ya Copa Amerika itachezwa jumapili ijayo Julai 25 mjini Lima,Peru.
Kombe la bara la Asia nalo lilifunguliwa jumamosi,lakini limekumbwa na patashika kati ya wenyeji China na Katibu mkuu wa Shirikisho la dimba la Asia Peter Velappan.katibu huyo aliwakasirisha wachina alipowatuhumu mashabiki wake kuonesha utovu wa heshima na adabu kwa kuzomea uwanjani wakati wa sherehe ya ufunguzi wa dimba hilo juzi jumamosi.China ilitoka sare 2:2 na Bahrein.Katibu mkuu Velappan alitishia kuzuwia mashindano makuu ya shirikisho la dimba la Asia kuchezwa tena mjini Beijing na kufika ubali wa kuelezea shaka shaka iwapo china itamudu kuandaa kwa mafanikio michezo ya olimpik 2008.Alisema " watu wa Beijing hawana adabu". Mashabiki wakizomea mbele ya rais wa FIFA Sepp Blatter,rais wa AFC-shirikisho la dimba la asia Mohammed Bin hammam na viongozi wa China.Na hii alisema katibu mkuu huyo si desturi ya mila za China."China ina utamaduni mkubwa,elimu ya juu lakini hii haikudhihirika leo"-alifoka Katibu mkuu wa Shirikisho la dimba la Asia.
Mashtaka hayo yamechochea lakini hasira miongoni mwa vyombo vya habari vya China na mashabiki:kikundi kidogo cha wakaazi wa Beijing kilimkabili Katibu mkuu Celappan mbele ya Hoteli yake na kumkabidhi barua ya malalamiko kwa matamshi aliotoa.Hata magazeti mjini Hong Kong yalimkosoa Velappan.
Katika dimba lenyewe, leo ni zamu ya Korea ya kusini kupambana na Jordan na Kuweit na umoja wa Falme za kiarabu.
Kombe la COSAFA-Castle Cup kusini mwa Afrika lilikuwa uwanjani mwishoni mwa wiki:Katika mpambano wa robo-finali mjini Luanda, Angola ilitoka suluhu na Botswana kwa kuachana jana bao 1:1 .
TUMALIZIE RIADHA:
Mashindano ya Olimpik ya athens yakikaribia mwezi ujao, wanariadha wa afrika wamekuwa wakijinoa mjini Brazzavile,Kongo:Afrika Kusini mwishoe jana yalipomalzika mashindano haya, iliibuka kileleni mwa orodha ya medali na kuipiku Kenya, muda mrefu ikipigiwa upatu kuwa Taifa kuu la riadha barani Afrika:
Afrika Kusini ilitwaa jumla ya medali 10 za dhahabu,12 za fedha na 8 za shaba.
Kenya ikija nafasi ya pili ilikusanya medali 7 za dhahabu, 7 za fedha na 5 za shaba.Nigeria ikafuata nafasi ya tatu kwa medali za dhahabu,3 za fedha na bila shaba.Wenyeji kongo walimaliza mkiani kwa medali 1 ya shaba. Ethiopia ilimaliza nafasi ya 6 nyuma ya tunisia kwa medfali 3 za dhahabu,4 fedha na 1 shaba.
Katika changamoto ya mita 1.500 wanawake,mkenya Nancy Lagat alinyakua ushindi akifuatwa na Mmorocco Saida El Mehdi.Jeruto Kiptum wa Kenya akaja nafasi ya 3.
Jana ilikua siku ya mwisho ya mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia kwa chipukizi-Junior Athletics Championship huko Grosseto,Itali.
Upande wa wanaume, Kiprono Choge alichukua ushindi katika masafa ya mita 5000 akimpiku muethjiopia Bado Worku na Tariku Bekele waliokuja nafasi ya pili na ya tatu.
Mashindano ya kukata tiketi za Olimpik kwa wanariadha wa Marekani,yalimalizika pia jana huko SACRAMENTO,California:
Kwa msangao wa mashabiki wengi, msichana mkongwe Gail Devers alikata tiketi yake kwa michezo yake ya 5 ya olimpik akiwa sasa na umri wa miaka 37.Devers alishinda mbio za mita 100 mkuruka viounzi na tiketi ya kwenda tena katika medani ya olimpik.