Brazil yashuhudia kampeni za mwisho kabla ya uchaguzi
1 Oktoba 2022Kampeni za kuwania urais nchini Brazil zitakamilika leo Jumamosi huku kukishuhudiwa upinzani mkali kati ya rais wa sasa na mgombea wa kambi ya siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro na Luiz Lula Da Silva kutoka kambi ya mrengo wa kushoto na ambaye aliwahi pia kuiongoza nchi hiyo kutoka mwaka 2003 hadi 2010.
Uchaguzi wa rais utafanyika kesho Jumapili huku nchi hiyo yenye uchumi mkubwa katika ukanda wa Amerika ya Kusini ikiwa imegawanyika.
Soma zaidi:Pazia la kampeni za uchaguzi wa rais lafunguliwa Brazil
Ili kupata ushindi mgombea atalazimika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Lula amekuwa akiandamwa na kashfa za ufisadi na alifungwa jela kwa miezi 18 kabla ya Mahakama ya Juu nchini Brazil kubatilisha hukumu hiyo mwaka jana.
Marekani imeshatowa onyo dhidi ya kutokea machafuko nchini Brazil ikisema itafuatilia kwa karibu kinachoendelea.Wapiga kura nchini Brazil sio tu watamchagua rais mpya lakini pia watapiga kura kuchagua wabunge wa bunge la taifa ,maseneta na magavana wabunge wa majimbo yote 27.
Bolsonaro amekuwa akitaja kuwa atayapinga matokeo ikiwa atashindwa huku akidai kuwa Mungu pekee ndie mwenye uwezo wa kumuoondoa madarakani na amekuwa akidai bila ya kuwa na ushahidi kwamba mfumo wa kupiga kura wa kieletroniki umezunguukwa na udanganyifu.
Baada ya uchaguzi huo utakaomalizika jioni saa kumi na moja kamili matokeo yanatarajiwa kutangazwa kiasi masaa mawili baadae.