1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil wapata pigo la Neymar

28 Novemba 2022

Brazil watalazimika kuwa bila mchezaji wao nyota Neymar katika mechi yao ya Jumatatu dhidi ya Uswisi, baada ya mchezaji huyo wa Paris Siant Germain kupata jeraha katika mechi yao ya kwanza walipocheza na Serbia.

Fußball Brasilien vs. Ghana Freundschaftsspiel
Picha: Mustafa Yalcin/AA/picture alliance

Lakini beki wa kati wa hao Selecao Marquinhos anasema kukosekana kwa Neymar, si mwisho wa mabingwa hao mara tano wa dunia.

"Tunajiamini kwa asilimia 100. Bila shaka tunatamani tungekuwa na Neymar na Danilo wakicheza na sisi, lakini tuko tayari na tuna imani kwa hiyo tutaonyesha kwamba kikosi chetu ni imara, tumejiandaa vyema na tunaweza kukabiliana na dhoruba zote zitakazotupata katika Kombe hili la Dunia," alisema Marquinhos.

Kwa upande wao Uswisi wanaamini kwamba wanao uwezo mkubwa wa kuwashusha mabega Brazil katika mechi yao ya leo.

Kocha Murat Yakin ambaye aliichezea timu hiyo ya taifa mara 49 anasema vijana wake wanacheza bila shinikizo lolote ila Brazil wanakabiliwa na shinikizo kubwa kwasababu lengo lao kuu ni kuondoka huko Qatar wakiwa mabingwa wa dunia.

Mshambuliaji wa Uswisi Breel EmboloPicha: Carl Recine/REUTERS

Yakin pia amezungumzia suala la kukosekana kwa mchezaji nyota wa Brazil Neymar katika mechi ya leo.

"Sitaki kumzungumzia mchezaji mmoja tu kwa wapinzani wetu, bila shaka ni mchezaji anayependwa, tunamuheshimu ila kwetu sisi hilo halibadilishi chochote, hilo halifanyi kazi yetu kuwa rahisi. Tunaitathmini timu kwa ujumla na iwapo mchezaji mmoja hachezi basi hatuhitaji kuzungumzia sana kuhusiana na hilo," alisema Yakin.