1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yaingiwa na kiwewe kabla ya pambano dhidi ya Chile

28 Juni 2014

Brazil ina wasi wasi kabla ya pambano lake la duru ya timu 16 katika kombe la dunia dhidi ya Chile leo Jumamosi(28.06.2014), wakati Uruguay inapaswa kujifunza kuishi bila Luis Suarez katika katika awamu ya mtoano.

Brasilianische Fußballfans
Mashabiki wa Brazil wanaiongezea mbinyo timu hiyoPicha: picture alliance/augenklick

Timu 16 zilizobakia katika kinyang'anyiro cha kombe la dunia bado hazijarejea katika hali ya kawaida baada ya michezo ya makundi, lakini duru ya pili inaanza mara moja ambapo wenyeji Brazil wanatiana kifuani na Chile mjini Belo Horizonte na Colombia ina miadi na Uruguay mjini Rio de Janeiro.

Kocha wa Brazil Luiz Felipe Scolari anatambua kuongezeka kwa mbinyo wa kucheza katika ardhi ya nyumbani.

Wachezaji wa BrazilPicha: picture alliance/augenklick

Wasi wasi upo

"Inaeleweka kwamba mtu anaweza kujisikia hali ambayo si nzuri na mhemko, hususan iwapo unaingia katika duru ya mtoano. Hatuwezi kuruhusu kufanya makosa ," Scolari amesema.

"Kuna hali kidogo ya shauku, na wasi wasi. Lakini hilo ni jambo la kawaida katika mashindano, sio kwasababu tuko nchini Brazil. Wakati nikiwa peke yangu na nikianza kufikiri, napata wasi wasi kidogo.

Nahodha wa Brazil Thiago Silva , mwenye umri wa miaka 29, amesema mbinyo ulianza katika mchezo wao wa ufunguzi ambapo walipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Croatia.

Brazil imeishinda Chile katika michuano yote mitatu waliyokutana katika kombe la dunia, ikiwa ni pamoja na ushindi wa mabao 3-0 katika duru ya mtoano ya timu 16 katika kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini.

Luiz Felipe Scolari kocha wa BrazilPicha: Reuters

Chile ni tofauti mara hii

Lakini huenda Brazil haijacheza na kikosi kigumu kama hiki cha Chile.

Alexis Sanchez na Artur Vidal wamekipa kikosi hicho nguvu ya ziada kama walivyoonesha ushindi wao dhidi ya Uhispania katika kundi B. Na Kocha Jorge Sampaoli anaihimiza zaidi na zaidi timu yake kushambulia.

Wachezaji wa Chile wakishangiria baoPicha: Getty Images

Sanchez amesema anaamini kikosi chao kitashinda " tumekuja hapa kuandika historia," amesisitiza.

Brazil haina hakika juu ya mlinzi wa kati David Luiz na Dante kutoka Bayern Munich huenda akapewa jukumu hilo katika kikosi hicho.

Mshindi atapambana na Colombia ama Uruguay katika robo fainali.

Na dunia itagundua mjini Rio ni kiasi gani marufuku aliyopigwa dhidi ya mshambuliaji Luis Suarez ya miezi minne kwa kumng'ata mpinzani wake kutoka Italia wiki hii jinsi ilivyoiathiri Uruguay.

"Tunafahamu uwezo walionao Uruguay na kila mchezo wanatoa kila tone la mwisho la jasho. Utakuwa mchezo wenye hisia nyingi, ambapo Uruguay itataka kufanya mambo kwa usahihi," amesema mlinda mlango wa Colombia David Ospina , ambaye huchezea soka nchini Ufaransa.

Kocha wa Uruguay Oscar Tabarez amepuuzia kutokuwepo Suarez.

"Tayari tumecheza michezo kadha bila Suarez," amesema.

"Tumeshinda baadhi , na tumepoteza baadhi, na hakuwapo dhidi ya Costa Rica pia."

Luis Suarez akiwa pamoja na Chiellini aliyemuumaPicha: picture-alliance/dpa

Colombia nayo ikiwa inamkosa Radamel Falcao kutokana na kuumia, mchezo huo mjini Rio unaweza kuwa mpambano kati ya wachezaji wanaochukua nafasi za wale ambao hawako Edinson Cavani kwa Uruguay na James Rodriguez kwa upande wa Colombia ambaye alipumzishwa wakati timu yake ikiirarua Japan kwa mabao 4-1 siku ya Jumanne.

Mchezo wa leo Jumamosi (28.06.2014) utakuwa wa kwanza ambao Uruguay inacheza mchezo wa kombe la dunia katika uwanja wa Maracana tangu walipoishangaza Brazil kwa kuishinda mabao 2-1 katika mchezo wa fainali katika mashindano ya mwaka 1950.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar