Brazil yajiandaa na mazishi ya Pele
3 Januari 2023Maelfu ya waombolezaji, wakiwemo wanafunzi wa shule za upili na majaji wakuu wa mahakama, walitoa heshima zao za mwisho jana Jumatatu mbele ya mwili wa Pele katika uwanja wa Vila Belmiro wenye uwezo wa kuwapokea watu 16,000. Kufikia saa 7 mchana jana Jumatatu, zaidi ya watu 27,000 walikuwa tayari wamelizunguuka jeneza ili kumuaga Pele.
Baadhi ya waombolezaji walilazimika kusubiri kwa saa kadhaa kwenye jua kali kabla ya kuuaga mwili wa yule aliyeitwa "Mfalme wa Soka."
"Nilisubiri kwa zaidi ya saa moja ili niingie, lakini nilishuhudia tukio la kihistoria. Kipaji cha Pele na historia aliyotengeza itabaki kuwa urathi. Alikuwa mtu muhimu sana.”
Soma zaidi: Ulimwengu wamuaga mwanasoka maarufu Pele
Misa ya kikatoliki itaadhimishwa katika uwanja wa Vila Belmiro kabla ya jeneza la Pele kupitishwa katika mitaa ya Santos na pia jirani na sehemu anakoishi mama yake mzazi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 100. Baadaye jeneza la Pele litapelekwa hadi kwenye mnara wa makaburi ya Necrópole Ecumênica yaliyo karibu na uwanja huo.
Katika miaka ya 1960 na 70, Pele alikuwa mchezaji maarufu zaidi duniani. Alikutana na viongozi wakuu kama marais na malkia, na nchini Nigeria vita vya wenyewe kwa wenyewe vilisitishwa kwa muda ili kumshuhudia Pele akicheza. Wabrazil wengi wanamsifu kwa kuiweka nchi yao kwenye jukwaa la dunia kwa mara ya kwanza.
Jina la Pele litadumu milele
Pele amefariki lakini jina lake litadumu milele. Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA Gianni Infantino aliwaambia waandishi wa habari kuwa kila nchi inapaswa kuwa na uwanja utakaokuwa na jina la Pele.
Kulingana na mamlaka nchini Peru, watoto 738 waliozaliwa mwaka jana, walisajiliwa kwa majina ya Pele, Mfalme Pele, Edson Arantes au Edson Arantes do Nascimento, jina kamili la gwiji huyo wa soka.
Soma zaidi:Maelfu wamuaga Pele
Pele mchezaji aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu mwaka 1958, 1962 na 1970, alifariki dunia Desemba 29 akiwa na umri wa miaka 82, kutokana na ugonjwa wa saratani ya utumbo. Pele kwa muda mrefu alikuwa mmoja wa wafungaji bora wa timu ya Brazil akiwa na mabao 77, lakini Neymar alivunja rekodi ya Pele wakati wa Kombe la Dunia huko nchini Qatar.