1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yakabiliwa na kiunzi cha Costa Rica

Daniel Gakuba
22 Juni 2018

Michuano ya kuwania kombe la dunia inaendelea nchini Urusi, macho yakielekezwa kwa Brazil ambayo inashuka dimbani na Costa Rica mjini Saint Petersburg, ikijaribu kuepuka kilichoifika Argentina hapo jana mbele ya Croatia.

Fußball WM 2018 Gruppe E Brasilien - Schweiz
Picha: Getty Images/AFP/J. Klamar

Brazil inaingia katika mechi ijayo ikijua fika kwamba matokeo yoyote mbali na ushindi, yataiacha katika nafasi ngumu kuweza kufaulu, na ugumu huo unazidishwa na ukweli kwamba wanakabiliana na Costa Rica ambayo iliipoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Serbia. Nahodha wa Brazil katika mechi ya leo, beki wa Paris St. Germain Tiago Silva, amesema inachotakiwa kufanya timu yake ni kutulia, na kila mmoja kufanya vizuri kadri ya uwezo wake.

Lakini Costa Rica ambayo katika michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2014 iliwashangaza wengi kwa kufika ngazi ya robo fainali, itakuja ikiwa imejizatiti, ikijua fika kuwa kushindwa mechi ya leo maana yake ni kuyaaga mashindano. Nahodha wake Bryan Ruiz amesema watajaribu kufuata nyayo za timu kama Croatia na Mexico, mbazo zimezitia kiwewe timu zilizokuwa zikipigiwa upatu za Argentina na Ujerumani.

Sampaoli akubali kubeba lawama

Lionel Messi, nyota yake katika mashindano ya kombe la dunia 2018 bado haijang'araPicha: Reuters/I. Alvarado

Bado gumzo kubwa katika vyombo vya habari na mitandaoni ni ubovu wa kikosi cha Argentina na nyota wake wa kimataifa kama Lionel Messi, Sergio Aguero na Gonzalo Higuain, na hususan kosa la kipuuzi la mlinda mlango Willy Caballero, ambalo lilisababisha goli la kwanza la Croatia. Lakini Kocha wa timu hiyo Jorge Sampaoli amesema anajitwisha lawama zote za matokeo mabaya.

''Ni kweli, mimi ndie nawajibika kwa maamuzi yote. Msingi kwa kushindwa kwetu ni jukumu langu kama kocha, ambaye niliwajibika kusuka mkakati wa kikosi. Ningekipanga tofauti na nilivyofanya, huenda matokeo yangekuwa mengine.'' Amesema Sampaoli na kuongeza kuwa hadhani ni sawa kumbebesha lawama zote Caballero.'

Kauli ya kocha huyo ambaye pia amesema kikosi chake hakikuweza kumtumia vyema Lionel Messi, imewachukiza wachezaji wengine ambao wameichukulia kama kuwalaumu kwa kipigo walichokipata. Alipoulizwa maoni yake kuhusu kauli hiyo, Sergio Aguero amesema, ''muache aseme chochote akitakacho''.

Kipi kitatokea kati ya Iceland na Nigeria?

Neymar wa Brazil, je leo atatamba mbele ya Costa Rica?Picha: Reuters/D. Sagolj

Argentia ambayo inaambulia pointi moja tu baada ya mechi mbili, nafasi yake finyu ya kusonga mbele itategemea matokeo kati ya timu nyingine katika kundi lake la D, kwa aina ya kipekee, yale kati ya mechi kati ya Nigeria na Iceland, ambayo inachezwa leo saa 12 jioni saa ya Afrika Mashariki.

Mechi nyingine itakayochezwa leo ni ile kati ya Serbia na Uswizi , itakayopigwa mjini Kaliningrad saa tatu usiku Afrika Mashariki. Miongoni mwa mashabiki wa Uswisi watakuwemo wale waliosafiri kwa trekta umbali wa km 1,800 kutoka kwao hadi mjini Kaliningrad wakitumia siku 14 kuja kushuhudia mpambano huo. Umbali huo ni kama kutoka Dar es Salaam hadi Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ukipitia Kigali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,dpae

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW