1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bremen kucheza nje ya uwanja wao

Josephat Charo
1 Mei 2020

Klabu ya Werder Bremen inayosuasua imesema inatafakari kucheza mechi zake za nyumbani katika mji mwingine nje ya uwanja wao wa Weserstadion iwapo Bundesliga itaanza tena mwezi Mei bila mashabiki kuwepo uwanjani.

Fußball DFB Pokal Achtelfinale SV Werder Bremen - Borussia Dortmund
Picha: picture-alliance/RHR-FOTO/D. Ewert

Janga la corona lilisababisha ligi ya Bundesliga kusitishwa katikati ya mwezi Machi huku Bayern Munich wakiwa kileleni na tofauti ya alama nne na Werder wakiwa katika nafasi ya pili kutoka mkiani. Ligi hiyo huenda ikarejea tena Mei 9 lakini mashabiki hawataruhiwa kutazama mechi viwanjani.

Serikali ya kansela Angela Merkel inasubiriwa kuidhinisha ligi irejee tena, lakini waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bremen, Ulrich Maeurer, amesisitiza hakuna mechi inayoweza kuchezwa katika uwanja wa Weserstadion wakati wa janga hili la corona. Hii ina maana Werder watalazimika kucheza mechi zao zilizosalia kwingineko, huku miji jirani iliyo na viwanja vyenye viwango vya mechi za Bundesliga, Hamburg, Hanover na Wolfsburg, ikifikiriwa.

"Kama, kwa sababu yoyote ile, hatutaweza kucheza Bremen, basi unatakiwa kuangalia maeneo mbadala," alisema afisa mkuu mtendaji wa Bremen, Klaus Filbry.

Mahusiano kati ya Werder na Maeurer yalivurugika kabla kuzuka janga la corona kwa kuwa mwanasiasa huyo amekuwa akitaka klabu hiyo ichangie gharama za kusimamia usalama wa mechi ambazo hukabiliwa na kitisho cha kuzuka machafuko.

Werder wako nje ya eneo salama la kutoshuka daraja kwa alama nane huku kukiwa kumesalia mechi tisa kabla msimu kukamilika. Hali yao ya kifedha imeathiriwa na janga la corona. Ijumaa wili iliyopita klabu hiyo ilithibitisha imechukua mkopo wa dharura na inatarajiwa kupata hasara ya euro zaidi ya milioni 40 msimu huu.

Mji wa Bremen uliifuta mechi kati ya Werder Bremen na Bayer Levekusen mnamo Machi 16 ambayo ilikuwa ichezwe bila mashabiki

(afpe)