1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bremen na Hamburg vitani kombe la UEFA

Aboubakary Jumaa Liongo7 Mei 2009

Leo usiku, kuna mechi za marudiano za nusufainali ya kombe la UEFA barani Ulaya, moja ni kati ya timu mbili za Ujerumani na nyingine ni kati ya timu mbili za Ukraine.

Kocha wa Bremen Thomas SchaafPicha: AP

Katika mechi inayozikutanisha timu za Ujerumani, Hamburg ikiwa na mtaji wa goli moja tena la ugenini, inaikaribisha Werder Bremen, ikijua fika kuwa mtaji huo hautoshi hata kama wanacheza nyumbani kuwa na hakika ya kufuzu kwa fainali.


Bremen iliitimua nje Hamburg katika nusufainali ya kombe la chama cha soka cha hapa Ujerumani iliyoamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, huku mlinda mlango wake Tim Wiese akizuia mikwaju mitatu ya Hamburg.


Pambano hilo la leo ni la nne kwa timu hizo hasimu kutoka Kaskazini mwa Ujerumani kukutana ndani ya kipindi cha siku 19.


Mara ya mwisho ilikuwa wiki iliyopita katika mechi ya kwanza ya nusufainali hiyo, ambapo ushindi wa Hamburg tena ugenini wengi wanaona ni nafasi kwao kulipiza kisasi kuitimua Bremen nje ya michuano hiyo, kama wao walivyotimuliwa katika michuano ya kombe la chama cha soka cha Ujerumani.


Lakini kocha wa Bremen Thomas Schaaf anaona kuwa bado wana nafasi ya kuitimua Hamburg.


´´Bilasha dunia iliyo mbele yetu hivi sasa siyo kubwa, ni sawa na mahali kwengine mtu anapoweza kufunga mabao matatu, manne , matano.Lakini bado kuna nafasi , lazima tuhakikishe Hamburg hawashindi mechi hii, sisi lazima tushinde´´.


Shabiki wa BremenPicha: AP

Bremen imekuwa na mwendo wa kinyonga katika Bundesliga ambapo mwishoni mwa wiki ililala mbele ya FC Köln kwa bao 1-0.


Hata hivyo mchezaji chipukizi wa timu hiyo ambaye kwa sasa yuko katika kiwango cha juu cha usukumaji kandanda hapa Ujerumani, kiungo Mesut Ozil anaungana na kocha wake Thomas Schaaf kuona nafasi iliyo mbele yao.


´´Nadhani bado tuna nafasi nzuri, tutatoa nguvu zetu zote´´.


Kwa upande wa Hamburg, baada ya kutimuliwa nje ya michuano ya kombe la chama cha soka cha Ujerumani, bado hata hivyo imeteleza katika mechi za hivi karibu za Bundesliga na iko katika hatari ya kukosa nafasi ya kucheza katika michuano ya vikombe vya Ulaya msimu ujayo, vinginevyo ishinde leo na kusonga mbele hata kutwaa ubingwa.


Piotr Trochwski ambaye alitia bao pekee la Hamburg katika mechi ya kwanza, ana hakika ya kuitimua Bremen na kucheza fainali tarehe 20 mwezi huu mjini Istanbul Uturuki


Mshambuliaji wa Hamburg Piotr TrochowskiPicha: AP

´´Ni dhahiri tuna nafasi nzuri kufutia ushindi wa bao 1 katika mechi ya kwanza.Hapa tunawashabiki nyuma yetu, tuliweza kuifunga bereme kwao breme, ndiyo maana hapa nyumbani tuna nguvu zaidi.Tuna uhakika kuwa tunashinda na kuweza kuingia fainali´´


Kocha Hamburg Martin Jol katika mechi ya leo ana furaha ya kurejea dimbani kwa mshambuliaji Mladen Petric ambaye alikuwa na maumivu.


Hamburg imewahi kushinda mara mbili vikombe vya Ulaya, ambapo mwaka 1977 ilishinda kombe la washindi na klabu bingwa mwaka 1983, wakati Bremen wao wameshinda mara moja kombe la washindi mwaka 1992.


Katika nusufainali nyingine ya michuano hiyo ya UEFA, Shahktar Donetsk inapigiwa upatu mkubwa kuweza kuwatimua wenzao Dynamo Kiev zote za Ukraine, kutokana na kuwa na mtaji wa goli la ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza .


Shahktar Donetsk haijawahi kushinda hata mara moja kikombe chochote cha ulaya, ambapo wapinzani wao Dynamo Kiev wamewahi kuwa mabingwa wa kombe la washindi mara mbili mwaka 1975 na 1986.


Kocha wa timu hiyo Mircea Lucescu anasema kuwa vijana wake kwa sasa hawana tena woga wa mechi kubwa, kwahivyo wana hakika ya kufuzu kwa fainali na kutwaa ubingwa


Mwandishi.Aboubakary Liongo

Mhariri.Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW