Brexit, bado mtihani kwa Theresa May
15 Novemba 2018Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May leo amekuwa katika harakati za kuunusuru mswada wa makubaliano ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, baada ya Waziri wake anayehusika na mchakato huo unaojulikana kama Brexit na mawaziri wengine kujiuzulu. Wote wanayapinga makubaliano hayo wakisema yatainasa Uingereza kwa miaka kadhaa ijayo.
Mbali ya waziri Dominic Raab anayehusika na mchakatao wa kujitoa Umoja wa Ulaya-BREXIT, wengine ni waziri wa kazi na malipo ya uzeeni Esther Mcvery , Naibu waziri anayehusika na Ireland kaskazini Shailesh Vara na naibu waziri wa Brexit Suella Braverman.
Hayo yamekuja wakati ambapo mwandishi mkuu wa masuala ya kisiasa wa gazeti la Daily Telegraph akiandika katika mtandao wake wa Twitte kwa kuzinukuu duru ambazo hazikutaka kutajwa jina, kwamba mbunge mkongwe Jacob Rees-Mogg anayepinga Uingereza kubakia Umoja wa Ulaya atawasilisha barua ya kutokuwa na Imani na bibi May.
Duru zinasema kutokana na kujiuzulu waziri Raab, Gavana wa Benki kuu ya Uingereza Mark Carney alitoa wito wakufanyika kikao cha vigogo wa masuala ya fedha pamoja na benki kubwa za Uingereza, baada ya sarafu ya Pound Sterling kushuka thamani na hisa katika masoko ya fedha kuteremka. Benki kuu mjini London ilikataa kusema lolote.
Akilihutubia bunge House of Commons leo, Waziri mkuu Theresa May alisema wamekuwa wakijitayarisha na hali ya kutopatikana makubaliano na wanaendelea kujitayarisha kwa hilo kwa sababu ametambua kwamba bado wanahatua nyengine ya majadiliano na Baraza la Ulaya, na baada ya makubaliano ya mwisho kupatikana yatapaswa kurudishwa bungeni.
May akaongeza kwamba chaguo liko wazi: "Uingereza inaweza kujitoa bila ya makubaliano au Waingereza kuungana na kuunga mkono kile alichokiita, makubaliano bora yatakayoweza kujadiliwa.”
Akijibu swali la mbunge mmoja , May amesisitiza:
"Hatutachukuwa chaguo alilosema la kubakia Umoja wa Ulaya, bali kwa hakika tutajitoa na hilo litatokea tarehe 29 Machi mwa ujao."
Naibu mkuu wa DUP Nigel Dodds, aliliambia bunge angeweza kurudia orodha ya ahadi lukuki ambazo waziri mkuu May alizitoa bungeni, na kwao wao faraghani kuhusu mustakbali wa Ireland Kaskazini katika uhusiano wa baadaye na Umoja wa Ulaya, lakini anahisi itakuwa ni kupoteza wakati, kwa sababu Bibi May ni mkaidi na ni wazi kwamba hasikilizi la mtu.
Nafasi ya bunge la Uingereza kuidhinisha makubaliano hayo kabla ya nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya Machi 29 mwaka ujao 2019, inaelekea inazidi kuwa ndogo. Akiungwa mkono na chama cha DUP cha Ireland Kaskazini , May ana wingi mdogo katika bunge la vita 650, lakini chama hicho sasa kinasema hakitoyaunga mkono makubaliano yaliofikiwa na Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters,AP
Mhariri: Iddi Ssessanga