1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Corbyn apanga kura ya kutokuwa na imani na serikali

Daniel Gakuba
15 Agosti 2019

Kiongozi wa chama cha Labour cha Uingereza, Jeremy Corbyn anadhamiria kuitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali ya waziri mkuu Boris Johnson kuzia mpango wa kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano.

Jeremy Corbyn
Picha: Reuters/T. Melville

Corbyn ameyasema hayo katika barua aliyowatumia viongozi wa vyama vingine vya kisiasa, na wapinzani wa Boris Johnson nani ya chama tawala, Conservative. 

Katika barua hiyo aliyoiandika jana Jumatano, Jeremy Corbyn alisema serikali inayoongoza Uingereza wakati huu haina ridhaa ya wananchi ya kuiondoa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya kiholela bila makubaliano yoyote. ''Kwa hiyo'', anaendelea Corbyn katika barua yake, ''Nadhamiria kuitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali haraka iwezekanavyo, pale tutakapopata uhakika wa kufanikiwa.''

Soma zaidi: Uingerea yaionya Ulaya kuhusu Brexit

Waziri Mkuu Boris Johnson ameapa kuheshimu muda wa mwisho kwa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya ambao ni tarehe 31 Oktoba mwaka huu, hata ikiwa hakutakuwa kumepatikana makubaliano yoyote ya uhusiano wa baadaye, katika mchakato ujulikanao maarufu kama Brexit.

Imani ya kumuangusha Johnson

Boris Johnson, Waziri Mkuu wa UingerezaPicha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Jeremy Corbyn alisema katika barua yake hiyo kuwa ikiwa kura yao ya kutokuwa na imani na serikali itashinda, atataka kuwekwa kama waziri mkuu wa muda mfupi ili kuweza kuzuia uwezekano wa Brexit ya kiholela. Baadaye alielezea imani kuwa kura hiyo itashinda.

''Natumai wote wataunga mkono kura ya kutokuwa na imani na serikali, kuhakikisha kwamba serikali hii haikurupukii brexit isiyo na mpango. Hilo litamaanisha kuwepo serikali ya muda chini ya uongozi wa chama cha Labour, ambayo itaitisha uchaguzi mkuu, ili watu wa nchi hii waamue mustakabali wao.'' Amesema.

Corbyn aliongezea kuwa akiwa waziri mkuu ataitisha uchaguzi mkuu, na angetaka kurefushwa kwa kipengele nambari 50 kinachohusu uanachama katika Umoja wa Ulaya.

Wananchi ndio wenye kauli

Msemaji wa ofisi ya waziri mkuu Boris Johnson amepinga azma hiyo hiyo ya Jeremy Corbyn, akisema serikali inaamini kuwa raia ndio wenye kauli ya mwisho, na maoni yao lazima yaheshimiwe. Amemtuhumu Corbyn kuamini kwamba watu ndio watumishi, na kwamba wanasiasa wanaweza kubatilisha matokeo ya kura zao ikiwa hawayafurahii.

Soma zaidi: Corbyn achaguliwa tena kuongoza chama cha Labour

Boris Johnson ambaye aliongoza kampeni ya kuondoka kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni ya mwaka 2016, na amefanya kuitenganisha nchi yake na umoja huo kwa namna yoyote ile, akiwapa changamoto wanasiasa wengine kuthubutu kumzuia.

Hapo jana alisababisha utata baada ya kusema wanasiasa wa Uingereza wanaopinga Brexit walikuwa wakishiriki katika kile alichokiita ''njama hatari'' na Umoja wa Ulaya. Kauli yake hiyo iliyokemewa vikali na wabunge wengi, aliitoa baada ya aliyekuwa waziri wa fedha Philip Hammond kutoka chama chake cha Conservative kusema kuwa bunge litasimama kidete kuzuia Brexit ya kiholela, na kuionya serikali ya Boris Johnson kuheshimu uamuzi huo.

 

rtre, dpae

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW