1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Brexit wajumbe bado hawajafikia makubaliano

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
20 Desemba 2020

Wajumbe wa Umoja wa Ulaya na wa Uingereza katika majadiliano ya Brexit hawajafaulu kufikia makubaliano ya biashara huku kila upande ukiutaka upande mwingine kulegeza masharti yake.

UK Großbritannien Symbolbild Brexit
Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Kizingiti kikubwa ni jinsi gani pande hizo mbili zitaendesha shughuli za uvuvi. Duru kutoka kwenye mazungumzo hayo zimesema suala hilo la uvuvi ndiyo jambo pekee linalozuia kufikiwa makubaliano kabla ya Januari mosi ili kuzuia kurejeshwa kwa kanuni za ushuru kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Bunge la Umoja wa Ulaya limesema muda wa mwisho wa kupatikana mkataba unapaswa kuwa usiku wa leo Jumapili tarehe 20.12.2020 ili kuwezesha mkataba huo kuidhinishwa kabla ya mwisho wa mwaka.

Soma zaidi: Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit

Uingereza imesisitiza kwamba iko tayari kujiondoa kutoka kwenye Jumuiya ya Ulaya bila ya mkataba wa kibiashara kuliko kuutia mtegoni uhuru wake huku kukiwa hakuna tamko lolote lililotolewa na makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuhusu hatua zilizopigwa kwenye mazungumzo ya siku nzima.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Tolga AkmenAFP/Getty Images

Wafanyabiashara nchini Uingereza wanahofia iwapo pande mbili hizo zitashindwa kufikia makubaliano ya biashara. Wamesema hali hiyo inaweza kusababisga wimbi la sintofahamu katika masoko ya fedha, na hivyo kuathiri uchumi wa bara Ulaya, kutatiza shughuli kwenye mipaka na matokeo yake yatakuwa ni kuvuruga mienendo  ya usambazaji wa bidhaa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ireland Simon Coveney amesema itakuwa vigumu kufikia makubaliano ya Brexit katika muda wa saa 24 zijazo na mazungumzo yote yanaweza kusambaratika kutokana kutofikiwa makubaliano juu ya swala la uvuvi.

Angalia: 

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya Brexit Michel Barnier amependekeza kwamba jumuiya hiyo itakuwa inarudisha asilimia 25 ya thamani ya samaki waliovuliwa kwenye bahari ya Uingereza, kikiwa ni kiwango kikubwa kuliko cha awali kilichopendekezwa na Umoja wa Ulaya lakini Uingereza imesema bado ni cha chini kulingana na matarajio yake.

Vyanzo: AFP/RTRE/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW