1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit na Uhamiaji ajenda kuu za Mkutano wa kilele wa EU

Caro Robi
19 Septemba 2018

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ameiambia Uingereza kuwa inahitaji kutafakari upya msimamo wake kuhusu suala la mpaka wa Ireland na mahusiano ya kibiashara katika siku za usoni baada ya Brexit.

Großbritannien, London: Symbolbild Brexit
Picha: Reuters/H. McKay

Akizungumza kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaoanza Jumatano mjini Salzburg, Austria, Tusk ameyakubali baadhi ya mapendekezo ya Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May lakini ameonya kuwa kuna masuala mengine kama hatma ya mpaka wa Ireland au mfumo utakaotumika wa ushirikiano wa kibiashara ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi upya.

Pande zote mbili zinatumai kufikia makubaliano kuhusu Brexit katika mkutano mwingine wa kilele wa Umoja wa Ulaya ili kuruhusu muda wa kutosha wa makubaliano hayo kuidhinishwa na bunge la Uingereza na Umoja wa Ulaya kabla ya Uingereza kujiondoa rasmi kuwa mwanachama wa Umoja huo mwezi machi mwaka ujao.

Lakini Tusk amesisitiza kuna haja ya kuwepo mkutano maalumu kati kati ya mwezi Novemba ili kuyaidhinisha yatakayokuwa yamekubaliwa kuhusu Brexit, akiongeza kuwa mazungumzo yanayoendelea yanaingia awamu muhimu mno na muda unazidi kuyoyoma.

Brexit na Uhamiaji masuala makuu

Umoja wa Ulaya pia umepokea vyema utayari wa Uingereza kuendelea kushirikiana katika masuala ya kimataifa hususan usalama na sera za kigeni. Kwa upande wake, May amewahimiza viongozi wa umoja huo kuunga mkono mpango wake kuhusu Brexit.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald TuskPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaert

Akihojiwa na gazeti la Ujerumani la Die Welt, May amesema Uingereza imeubadilisha msimamo wake wa awali na hivyo kuna haja kwa Umoja wa Ulaya pia kufanya hivyo.

Huku ikiwa imesalia miezi sita kabla ya nchi hiyo kujiengua kabisa kutoka Umoja wa Ulaya, bado kunasalia masuala muhimu ambayo hayajatatuliwa, lakini May anasema makubaliano yanaweza kufikiwa iwapo tu pande zote zitaonesha utashi wa kufanya hivyo.

Mbali na suala hilo la Brexit, mkutano huo wa kilele wa Salzburg utakaokamilika hapo kesho, utajadili suala tete la uhamiaji. Donald Tusk amesema muda umewadia wa kukomesha mivutano na malumbano kuhusiana na suala hilo na viongozi kukoma kulitumia kujinufaisha kisiasa.

Uhamiaji unabashiriwa utaghubika ajenda nyingine za mkutano huo. Licha ya kuwa idadi ya wakimbizi na wahamiaji waliowasili kusini mwa Ulaya mwaka huu imepungua, suala la uhamiaji limerejea tena katika ajenda za kisiasa za mataifa kadhaa ya umoja wa Ulaya.

Italia, Austria, Hungary na Ujerumani suala hilo limekuwa likifukuta na kuibua wasiwasi wa kuyapa nguvu makundi na vyama vya misimamo mikali ya mrengo wa kulia.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW