1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Suala la mpaka wa Ireland bado halijapata ufumbuzi

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
6 Machi 2019

Mazungumzo baina ya mwanasheria mkuu wa Uingereza na Umoja wa Ulaya juu ya kuleta mabadiliko zaidi kuhusu suala la mpaka wa Ireland yamemalizika bila ya makubaliano.

Brüssel Statement EU Brexit Unterhändler Barnier
Picha: picture-alliance/Xinhua/Y. Pingfan

Baada ya kukutana kwa muda wa saa zaidi ya tatu mjini Brussels wajumbe wa Uingereza na wa Umoja wa Ulaya walimaliza mazungumzo yao bila ya kukubaliana. Ujumbe wa Uingereza uliongozwa na mwanasheria  mkuu wa nchi hiyo Geoffrey Cox ulikutana na mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier kuzungumzia uwezekano wa kuleta mabadiliko katika suala la mpaka wa Ireland.  Hata hivyo duru za pande zote mbili zimesema kuwa mazungumzo mengine yataendelea leo.

Uingereza inatarajiwa kuondoka Umoja wa Ulaya itakapofika tarehe 29 mwezi huu lakini sasa pana mashaka iwapo hatua hiyo itawezekana, kutokana bunge la Uingereza kuukataa mkataba uliowasilishwa na waziri mkuu Theresa May mnamo mwezi Januari. 

Mwanasheria mkuu Goffrey Cox na waziri anaehusikana mchakato wa Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya Brexit - Stephen Barclay, wamepewa jukumu na waziri  mkuu Theresa May kujaribu kukibadilisha kipengele kinachohusu mpaka wa Ireland katika mkataba uliokwishafikiwa  baina ya Umoja  wa Ulaya na Uingereza. Kipengele hicho kinahakikisha kuwepo mpaka wazi baina ya Ireland kaskazini na  Jamhuri ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/AP Photo/UK Parliament/M. Duffy

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza bwana Barnier alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa uhakikisho zaidi ili mkataba uliofikiwa baina ya jumuiya hiyo na waziri mkuu Theresa May uweze kupitishwa bungeni. Bwana Barnier pia amedokeza kuwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaweza kukubali pendekezo la kuisogeza mbele tarahe ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.

Waziri anayeshughulikia mchakato wa Brexit Stephen Barclay hakusema kitu chochote baada ya mazungumzo kumalizika mjini Brussels. Hata hivyo hapo awali waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jeremy Hunt alisema Uingereza bado inataka kuondoka Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi huu lakini inategemea iwapo makubaliano yatapatikana haraka.

Wakati huohuo wawakilishi wa Umoja wa Ulaya na Uingereza wamesema mabadiliko yanaweza kufikiwa kama sehemu ya nyongeza katika mkataba. Serikali ya  waziri mkuu May inatumai mabadiliko hayo yatatosheleza kuwafanya wabunge wa nchi yake wabadilishe msimamo wao. Wabunge waUingereza  wamegawanyika kwa kiwango kikubwa juu ya suala la Brexit. 

Vyanzo: AFP/RTRE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW