Brexit: Theresa May akabiliwa na shinikizo
6 Julai 2018Waziri Mkuu Theresa May leo aliongoza mkutano wa baraza lake la mawaziri ili kuujadili mpango wa Uingereza wa kujiondoa Umoja wa Ulaya. Bibi May alitumai kuweza kuikamilisha sera ya nchi yake juu ya uhusiano wa hapo baadaye baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya katika masuala ya ushuru na masoko.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa, waziri mkuu huyo alikabiliwa na kile kilichobainika kuwa dalili za uasi mkubwa dhidi yake kutoka kwa mawaziri wanaounga mkono uamuzi wa Uingereza wa kujiondoa Umoja wa Ulaya. Mawaziri wapatao 30 walihudhuria mkutano huo bila ya kuruhusiwa kuingia na simu zao. Wakati imebakia miezi tisa tu kabla ya Uingereza kujiondoa kabisa Umoja wa Ulaya, Bibi May aliwaambia mawaziri wake kuwa Uingereza ina fursa kubwa lakini pia ina wajibu wa kukubaliana juu ya mpango wa Brexit.
Ripoti kutoka jijini London zinasema kuwa mpango huo wa Brexit uliowasilishwa na Bibi May kwa mawaziri wake ulitiliwa mashaka na baadhi ya mawaziri hao, ikiwa pamoja na waziri wake wa mambo ya nje Boris Johnson. Mawaziri hao wanasema mpango utaifanya Uingereza iendelee kuwa karibu sana na sheria za Umoja wa Ulaya juu ya biashara na bidhaa.Mawaziri hao wanahoji kuwa mpango uliowasilshwa na waziri mkuu wao utapunguza uwezo wa Uingereza wa kuingia katika mikataba mipya ya kibiashara na Marekani na nchi nyingine duniani.
Hapo jana mawaziri kadhaa wanaounga mkono Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya ikiwa pamoja na Boris Johnson walikutana kwa faragha na hivyo kusababisha uvumi kwamba mawaziri hao huenda wakajiuzulu nyadhifa zao ikiwa waziri mkuu hatalibadilisha pendekezo lake la kurasa 120. Hata hivyo waziri mwandamizi David Lidington ambae takriban ni makamu wa bibi May amesema anatumai mwafaka utapatikana kwenye mazungumzo ya leo. Kwa upande mwengine, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza, Michel Barnier amesema yapo maswali mengi yanayopaswa kujibiwa na Uingereza juu ya mpango wa nchi hiyo wa kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.
Barnier ameelezea masuala kama vile ulinzi wa data, ushirikiano kati ya polisi pamoja na mamlaka ya mahakama na usimamizi wa mkataba wa kujiondoa Uingereza kutoka kwenye Umoja wa Ulaya kama masuala tete yanayohitaji ufumbuzi kati ya pande hizo mbili
Katika hatua nyengine, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Horst Seehofer alisababisha hasira pale alipowasilisha barua ambayo inaonya kuwa msimamo mkali wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Uingereza unaweza kuhatarisha usalama wa raia wa Umoja huo.
Msemaji wa Tume ya Ulaya, Natasha Bertaud alisisitiza kuwa kuna mzungumzaji rasmi mmoja tu anayehusika na suala la Brexit ambaye ni Michel Barnier, huku msemaji wa Barnier akiliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kwamba hoja ya Seehofer siyo msimamo wa Baraza la Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/AP
Mhariri: Mohammed Khelef