Waengereza wajuta baada ya Brexit
27 Juni 2016Kura ya maoni ya Uengereza ambapo karibu asili mia 52 wamekubali nchi yao ijitoe katika Umoja wa Ulaya , imebainisha jinsi jamii nchini Uingereza ilivyogawika-linaandika gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaloendelea kuandika:"Kura ya Brexit si ya nadra. Inabainisha mfarakano uliopo kati ya matajiri na maskini,kati ya wazee na vijana na pia mtengano kati ya majimbo ya nchi hiyo. Katika wakati ambapo wakaazi wa Wales na England-ikitengwa London,wanapinga nchi yao kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya,wenzao wa Scottland na Ireland ya kaskazini wamepiga kura kwa wingi Uingereza isalie kuwa mwanachama. Kura yao ya "Bremain" ilikuwa bayana kwa namna ambayo imeutia kishindo kikubwa mfumo wa demokrasia wa nchi hiyo. Kambi ya washindi ya wahafidhina-Tories na chama cha siasa kali za kizalendo-UKIP wanataka kuiona Uingereza ikirejea tena kuwa na usemi mkubwa duniani. Mwishoe lakini watakaotawala ni pepo wadogo wadogo na nchi inazongwa na kishindo cha kugawanyika.
Umoja wa ulaya unataka zoezi la kujitoa lianze mara moja
Hakuna kinachodhihirisha mtengano katika jamii ya Uingereza kama malalamiko yaliyoandikwa mtandaoni ambapo kufumba na kufumbua zaidi ya waingereza milioni tatu,wengi wakiwa vijana wanataka,kura nyengine ya maoni iitishwe ili watu waamue kama wanataka Brexit iidhinishwe au ibatilishwe. Wakati Uingereza kunatokota,Umoja wa Ulaya unatia kishindo kutaka maombo yaharakishwe. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika: "Ni sawa kabisa kwamba sasa Bruxels inahimiza mambo yamalizwe haraka haraka. David Cameron amezikera taasisi za Umoja wa Ulaya alipojaribu kuvuta wakati akisema eti watu waanze kuagana ifikapo msimu wa mapukutiko mwaka huu. Hadi wakati huu waziri mkuu huyo anaebidi kung'atuka,amekuwa akikubaliwa takriban kila alichokitaka-kwasababu wenzake walitaka kuiridhisha Uingereza ili iendelee kuwa mwanachama. Enzi hizo zimekwisha hivi sasa. Maombi rasmi ya kujitoa katika Umoja wa ulaya,yanabidi yatolewe wiki hii ili kuepusha madhara ya Brexit yasienee katika sekta nyengine baada ya masoko ya hisa. Majadiliano yatakayofuatia hayatakiwi yatoe picha kana kwamba Cameron na wenzake wameahidiwa bahashishi-kwasababu hali kama hiyo inaweza kuzishawishi nchi nyengine pia zifuate nyayo za Uingereza na kwa namna hiyo kusababisha kuvunjika muungano wa ulaya.
Papa Francis azungumzia kuhusu mauwaji ya halaiki ya waarmenia
Mada ya mwisho magazetini inahusu ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis nchini Armenia.Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika: "Papa Francis ni mtu anaejulikana,hatafuni maneno. Kwamba sasa anajitafutia lawama za Uturuki alipoyataja mauwaji ya Armenia yaliyotokea miaka zaidi ya miaka moja iliyopita,kuwa ni mauwaji ya halaiki,hilo analijua fika. Hata hivyo matamshi yake yamewalenga wengine pia; wenyeji wake,waarmenia,kwa kuzingatia hali namna ilivyo hivi sasa. Kwasababu Papa Francis amewatolea na wao pia wito,maovu yaliyotendwa miaka ya nyuma dhidi ya wananchi wake wenyewe yatumiwe kama funzo ili kutoendelea kupalilia mzozo wake wa sasa pamoja na jirani yake Azarbaijan. Kwasababu nchi hizo mbili zinajikuta katika hali inayofanana na vita ambapo watu zaidi ya 100 wameshauwawa tangu mwezi wa April mwaka huu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu