1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

BRICS: Putin asema kuishinda Urusi ni ndoto isiyofikirika

24 Oktoba 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya juu ya mawazo ya kuishinda Urusi kwenye uwanja wa vita na ameyaita kuwa ni ndoto. Ameyasema hayo kabla ya mkutano wake wa kwanza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Russland BRICS I Wirtschaftsforum, Moskau mit Präsident Putin
Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza hayo katika mkutano wa kilele wa BRICS ambao leo Alhamisi Oktoba 24, ni siku ya mwisho ya mkutano huo.

Putin na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wanakutana baada ya muda wa zaidi ya miaka miwili na wanatarajiwa kuuangazia mzozo wa Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimir Putin akihutubia katika siku ya mwisho ya Mkutano wa BRICS alitoa maoni yake juu ya mzozo wa Ukraine. Amesema vita hivyo ni matokeo ya vitendo vya "nguvu zinazotumiwa kwa mantiki ya kuwatawala watu wote".  Putin amesema Ukraine inatumiwa kujenga vitisho vya kimkakati kwa Urusi.

Kushoto: Rais wa China Xi Jinping. Kulia: Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Putin amesema: - "Ukraine ni moja ya mifano hiyo. Ilitumika na imekuwa inatumika kutengeneza vitisho vya kimkakati kwa Urusi,lakini wakati huohuo wanasahau masilahi yetu muhimu, wasiwasi wetu wa haki na ukiukaji wa haki za watu wanaozungumza lugha ya Kirusi. Lazima niseme kwamba hii ni ndoto iliyojaa udanganyifu ambayo labda inaweza kuaminiwa na wale ambao hawaijui historia ya Urusi, hawajali umoja ulioundwa kwenye karne nyingi, nguvu ya imani na mshikamano wa watu wake.”

Soma Pia: BRICS yataka vita vikomeshwe Gaza, Ukraine 

Rais wa Urusi amesema kambi ya BRICS itasaidia kuunda umoja wa nchi zinazoinukia kiuchumi kushindana na nchi Magharibi ambazo zinaonesha waziwazi lengo la kutaka kuishinda Urusi kwa kutumia njia za kimkakati.

Urusi pia imesisitiza kuundwa kwa mfumo mpya wa malipo ambao utatoa njia mbadala ya huduma za benki kimataifa badala ya mfumo wa SWIFT unaosimamiwa na Marekani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuwepo kwa "amani na haki" nchini Ukraine katika mkutano huo wa viongozi wa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi BRICS ulioandaliwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mazungumzo ya Putin na Guterres yanafanyika wakati ambapo wanajeshi wa Urusi wanaendelea kusonga mbele katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine, wakikaribia karibu na kituo kikuu cha usambazaji cha Pokrovsk.

Ukraine imelaani ziara ya Guterres nchini Urusi, huku wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ikimlaumu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kukubali kukutana na Putin.

Viongozi kadhaa wa dunia wametoa wito wa kusitishwa mzozo kati ya Urusi na Ukraine katika mkutano wa kilele wa BRICS. Rais Xi Jinping wa China ametahadharisha juu ya kutokea "changamoto kubwa" duniani na amesema anatumai kwamba nchi za BRICS zinaweza kuwa "nguvu ya kuleta utulivu".

Katikati;: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa. Kulia Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Alexander Nemenov/Pool via REUTERS

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema anataka mzozo huo utatuliwe "kwa amani". Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa pia amema nchi yake inaunga mkono kikamilifu juhudi za kurejesha amani na utulivu kwa haraka.

Jukwaa la BRICS lilianzishwa miaka 15 iliyopita na nchi zinazoinukia kiuchumi Brazil, Urusi, India, China na  Afrika Kusini, na zimezijumisha nchi za Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu. Azerbaija na Malaysia zimeomba kujiunga na kambi hiyo.

Soma Pia: Putin: BRICS itachochea ukuaji wa uchumi duniani  

Uturuki pia imeelezea dhamira yake ya kutaka kujiunga na kundi la BRICS. Rais Recep Tayyip Erdogan amesema anataka Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya NATO iwe ya kwanza kujiunga na BRICS. Erdogan amehudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa rais wa Urusi Vladimir Putin baada ya kuomba mwezi uliopita kujiunga na umoja huo.

Vyanzo: AFP/AP