1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

BRICS yajadili uwezekano wa kujitanua

2 Juni 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Ma Zhaoxu pamoja na wanadiplomasia wengine wa ngazi ya juu wa Jumuia ya Nchi Zinazoendelea Kiuchumi, BRICS.

Südafrika Treffen der BRICS-Außenminister in Kapstadt
Picha: Foreign Ministry Press Service/ITAR-TASS/IMAGO

Mkutano huo wa wanadiplomasia wa BRICS uliangazia uwezekano wa jumuia hiyo kujitanua na kuzijumuisha nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani, ikiwemo Saudi Arabia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Kabla ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Alhamisi katika hoteli ya kifahari iliyoko kando ya bahari kwenye mji wa Cape Town, Afrika Kusini, Lavrov ameiweka BRICS ambayo kwa sasa inazijumuisha nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, kama msingi wa kuanzishwa kwa utaratibu wa ''haki zaidi'' ulimwenguni.

Nchi za Magharibi na vikwazo

Lavrov pia ameyakosoa mataifa ya Magharibi kutokana na vikwazo vyake pamoja na kile alichokiita hujuma za vitisho katika soko la fedha dhidi ya Urusi.

''BRICS ina muundo tofauti. Ni shirika jipya linalozingatia kanuni za usawa, kuheshimiana, maafikiano na kutoingiliana. Jumuia hii inazingatia kikamilifu Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kwa kufuata kanuni zake zote za kuanzisha jumuia,'' alisisitiza Lavrov.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Vyacheslav Prokofyev/TASS/IMAGO

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor mwenyeji wa mkutano huo, amethibitisha kuwa Rais wa Urusi, Vladmir Putin amealikwa Afrika Kusini katika mkutano wa kilele wa BRICS utakaofanyika mwezi Agosti, licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kutoa waranti wa kukamatwa kwake.

Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi, Brazil, India, Afrika Kusini na China, ulikuwa maalum kwa ajili ya kuandaa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za BRICS utakaofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini, na umefanyika chini ya wiki mbili baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 nchini Japan.

Kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi kama adhabu kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine na kutafuta njia za kukabiliana na ushawishi wa kiuchumi wa kimataifa wa China ulimwenguni kulitawala mkutano huo wa G7 uliofanyika Hiroshima.

Viongozi wa G7 wakiwa na Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Susan Walsh/REUTERS

Lavrov amesema kutokana na hali iliyojitokeza ya hatua zilizochukuliwa na nchi za Magharibi, nchi zao zinapaswa kutafuta kikamilifu majibu ya pamoja kwa changamoto za wakati huu. Kutokana na ushiriki wa Urusi na China, BRICS inazidi kutazamwa kama kigezo kinachoibuka kwa G7 na mataifa ya Magharibi, na upanuzi wa jumuia hiyo unaweza kuimarisha ushawishi wa kisiasa na kiuchumi wa Urusi na China.

Wanadiplomasia wa nchi 15 waalikwa mkutano wa Ijumaa

Balozi wa Afrika Kusini katika jumuia ya BRICS, Anil Sooklal amesema zaidi ya nchi 20 zimeomba rasmi na kwa njia isiyo rasmi kujiunga na jumuia hiyo. Sooklal anasema Saudi Arabia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu kila mmoja ametuma maombi rasmi ya kujiunga na BRICS.

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kwenye takribani nchi 15, baadhi yao zikiwa zilizoomba kuwa wanachana wapya wa BRICS, wamealikwa Ijumaa, katika siku ya pili ya mkutano wa wanadiplomasia wa BRICS

(DPA, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW