1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRICS yazinduwa Benki Mpya ya Maendeleo

16 Julai 2014

Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi BRICS yameanzisha benki ya maendeleo yenye thamani ya dola bilioni 100 katika hatua ya kuubadili mfumo wa fedha wa kimataifa unaohodhiwa na mataifa ya magharibi.

Viongozi wa nchi za BRICS wakati wa uzinduzi wa Benki Mpya ya Maendeleo huko Fortaleza, Brazil . (15.07.2014)
Viongozi wa nchi za BRICS wakati wa uzinduzi wa Benki Mpya ya Maendeleo huko Fortaleza, Brazil . (15.07.2014)Picha: Reuters

Viongozi wa mataifa hayo yanayoinukia kiuchumi BRICS yamezinduwa benki hiyo katika mkutano wa Viongozi wa kundi hilo la BRICS mjini Fortaleza - Brazil Jumanne (15.07.2014).

Benki hiyo inayokusudia kugharamia miradi ya miundo mbinu katika nchi zinazoendelea makao yake makuu yatakuwa mjini Shanghai China na India itasimamia shughuli zake kwa miaka mitano ya kwanza ikifuatiwa na Brazil na baadae Urusi.

Viongozi wa mataifa ya BRICS pia wameunda mfuko wa akiba utakaokuwa na uwezo wa dola bilioni 100 kukabiliana na shinikizo za kifedha.Benki hiyo ilokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu itaitwa Benki ya Mpya ya Maendeleo.

Hayo ni mafanikio ya kwanza makubwa ya nchi zinazounda BRICS za Brazil,Urusi,India,China na Afrika Kusini tokea zilipokutana mwaka 2009 kushinikiza kuwa na sauti kubwa katika mfumo wa fedha duniani ulioanzishwa na mataifa ya magharibi baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kujikita katika Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Benki ya Dunia.

Ushawishi wa BRICS

Mataifa hayo yanayoinukia kiuchumi yalilazimika kuratibu hatua hiyo ya pamoja kufuatia kuhamishwa kwa mtaji kutoka katika nchi zinazoinukia kiuchumi mwaka jana kulikosababishwa na hatua za kuchochea uchumi za Marekani.

Viongozi wa nchi za BRICS wakiwa Fortaleza, Brazil . (15.07.2014)Picha: Reuters

Benki hiyo mpya inaonyesha kuongezeka kwa ushawishi wa mataifa hayo yanayounda BRICS ambayo kwa jumla yana nusu ya idadi ya watu duniani na pato la kiuchumi duniani la takriban asilimia 20.

Benki hiyo itaanza na mtaji wa kuandikisha wa dola bilioni 50 ukigawiwa sawa sawa kati ya mataifa mtano waasisi wa BRICS na dola bilioni 10 taslimu zitakazotolewa awali katika kipindi cha miaka saba pamoja na dhamana za dola bilioni 40. Benki hiyo itaanza kutowa mikopo hapo mwaka 2016 na kupokea wanachama wa nchi nyengine lakini mgao wa mtaji wa mataifa ya BRICS katika benki hiyo haupaswi kushuka na kuwa chini ya asilimia 55.

Mbadala wa ushawishi wa Marekani

Taasisi hiyo inabidi iridhiwe na mabunge wa nchi za BRICS.

Viongozi wa nchi za BRICS katika Mkutano wa Kilele Fortaleza, Brazil . (15.07.2014)Picha: Reuters

Rais Dilma Rousseff wa Brazil ameweka wazi uwezekano wa kutumia fedha za benki hiyo kuzisaidia nchi nyengine ambazo sio wanachama wa BRICS.

Leo viongozi wa mataifa hayo ya BRICS watakuwa na mkutano wa kilele na marais wenzao wa Amerika Kusini kutafuta njia mbadala za kukabiliana na ushawishi wa Marekani katika eneo hilo la Amerika Kusini.

Mataifa yatakayohudhuria mkutano huo ni pamoja na Argentina,Chile,Colombia, Ecuador na Venezueala.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman