BRUSSELS. Paul Wolfowitz auhakikishia Umoja wa Ulaya kuwa kazi ataiweza.
30 Machi 2005Mteule wa Marekani katika wadhfa wa rais wa benki ya dunia Paul Wolfowitz ameuhakikishia ujumbe wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya kuwa uteuzi wake kutetea kiti hicho hauna kasoro yoyote.
Akizungumza hayo baada ya mkutano na mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya huko Brussels, Wolfowits amesisitiza kuwa benki ya dunia ni chombo muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya umaskini.
Kuteuliwa kwa Paul Wolfowitz waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani na mshika bendera ya uvamizi wa Iraq ukiongozwa na serikali ya rais George Bush wa Marekani, kumezusha manung’uniko miongoni mwa wanasiasa wa Ulaya.
Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani bibi Haidemarie Wieczorek-Zeul amesema kuwa mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanataka hakikisho kuwa rais mpya wa benki ya dunia atalipa kipaumbele swala la kuupiga vita umasikini.