BRUSSELS: Ujerumani yatakiwa kuongeza juhudi kupambana mabadiliko ya hali ya hewa
7 Aprili 2007Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na mazingira, Stavros Dimas, ameitaka Ujeumani iongeze juhudi zaidi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mwito huo umetolewa siku moja tu baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kutolewa.
Ripoti hiyo ilisema ongezeko la joto duniani litaathiri zaidi nchi maskini. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu jopo la kiserikali linalohusika na mabadiliko ya hali ya hewa mjini Brussels lilikubaliana juu ya vifungu vya maneno katika ripoti hiyo inayosema mabadiliko ya hali ya hewa yanayosabishwa na utoaji wa gesi za viwandani yamefikia kiwango cha juu.
Ripoti hiyo inasema kuenea kwa jangwa, ukame na kuongezeka kwa viwango vya maji katika bahari, kutaathiri maeneo ya nchi za joto barani Afrika hadi visiwa vya bahari ya Pacific.
Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amezieleza juhudi za Marekani na China kuviondoa baadhi ya vifungu katika ripoti hiyo kuwa kashfa. Amezishutumu nchi hizo kwa uharibifu wa kisayansi na kuongeza kusema kwamba watu wana haki ya kujua kuhusu matokeo halisi ya mabadiliko ya hali ya hewa.