1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Ulaya yaunga mkono ulinzi wa Marekani

20 Aprili 2007

Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO waunga mkono mpango tata wa Marekani kuanzisha mfumo wa makombora ya kujihami Ulaya ya mashariki.

Katika mkutano wao mjini Brussels nchini Ubelgiji nchi wanachana wa NATO pia zimekubali kwamba mfumo wowote ule wa makombora ya kujihami wa NATO wa kipindi cha usoni ujalizie ule wa Marekani ili kuhakikisha kwamba Ulaya nzima imepata ulinzi huo.

Hata hivyo serikali ya Urusi imeendelea kupinga wazo la kuwa na mfumo wa makombora ya kujihami wa Marekani katika nchi jirani zake na imekuwa ikiishutumu serikali ya Marekani kwa kuilenga Urusi.

Marekani inasistiza kwamba uwekaji wa mfumo huo nchini Poland na katika Jamhuri ya Czeck hautokuwa tishio kwa Urusi na kwamba unaweza kutumiwa kulinda sehemu za Ulaya dhidi ya makombora yoyote yale yatakayofyatuliwa kutoka Mashariki ya Kati.