BRUSSELS: Umoja wa Ulaya wakubali kutuma wanajeshi kusini mwa Lebanon
24 Agosti 2006Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya watakutaka kesho mjini Brussels kujadili michango yao katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani kusini mwa Lebanon.
Umoja wa Ulaya ulikubali jana kuchangia kikosi kikubwa cha wanajeshi katika jeshi la Umoja wa Mataifa litakalopelekwa Lebanon.
Akizungumza juu ya kikosi hicho waziri mkuu wa Itali, Romano Prodi, alisema, ´Tunategemea uamuzi wa Umoja wa Mataifa. Tunajiandaa kwa kazi hiyo. Ikihitajika na ikiamuliwa, tutaweza kuanza katika kipindi kifupi kwa kweli, kwa sababu pia kijiografia tuko karibu na Lebanon.´
Itali imesisitiza kujitolea kwake kutategemea mchango wa Umoja wa Ulaya na imezitolea mwito nchi wanachama wa umoja huo zijitolee kikamilifu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Itali, Romano Prodi, mjini Roma baadaye leo kujadili tume ya amani ya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon.
Wakati haya yakiarifiwa, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anajiandaa kuzuru Mashariki ya Kati hapo kesho. Msemaji wake amesema atazitembelea Israel, Lebanon, Syria na Iran.