1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Umoja wa Ulaya yataka utulivu Togo

30 Aprili 2005

Umoja wa Ulaya umetowa wito wa kuwepo kwa utulivu katika Jamhuri ya Afrika magharibi ya Togo kufuatia machafuko ya siku kadhaa yaliochochewa na matokeo tata ya uchaguzi yaliomtangaza mshindi mtoto wa Rais wa zamani wa nchi hiyo.

Umoja wa Ulaya umeelezea wasi wasi mkubwa juu ya machafuko hayo ambayo kwa mujibu wa repoti ya ubalozi wa Marekani kwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo yamepelekea kuuwawa kwa takriban watu 100 tokea tume ya uchaguzi ilipotangaza hapo April 24 kwamba Faure Gnassingbe ameshinda uchaguzi wa nchi hiyo.

Ujerumani hapo jana imewataka raia wake kuondoka Togo kufuatia machafuko hayo na kuripuliwa kwa moto kwa kituo chake cha utamaduni mjini Lome.

Mapema hapo jana Ujerumani ililaani shambulio hilo kwa kituo cha Goethe Institute ambacho kimeteketezwa kabisa baada ya watu wenye silaha kukifyatulia risasi.Ujerumani ambayo ilikuwa mkoloni wa Togo kwa miaka 30 hadi hapo mwaka 1915 imetaka uchunguzi ufanyike juu ya shambulio hilo.

Serikali ya Togo hivi karibuni imekuwa ikiushutumu vikali ubalozi wa Ujerumani kwa madai ya kuunga mkono upinzani.Waziri wa zamani wa mambo ya ndani Francois Esso Boko ambaye alitowa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo na baadae kutimuliwa kwenye wadhifa wake hivi sasa amejihifadhi kwenye ubalozi wa Ujerumani.

Wakati huo huo upinzani nchini Togo umesema hapo jana kuwa uko tayari kuwa na mazungumzo na wasuluhishi wa kimataifa kukomesha mgogoro huo na mataifa ya Afrika yanayounda Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS leo yanatazamiwa kupeleka ujumbe wa ngazi ya juu katika mji mkuu wa nchi hiyo Lome na kuonya kwamba mapigano baada ya uchaguzi nchini humo yanatishia utulivu wa eneo zima la Afrika Magharibi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW