Bucharest. Kesi mpya za virusi vya mafua ya ndege.
20 Oktoba 2005Nchi kadha katika bara la Ulaya na Asia zinaripoti kutokea upya kwa virusi vya homa ya mafua ya ndege miongoni mwa mifugo ya kuku na bata pamoja na ndege wengine, na kuzusha wasi wasi mpya kuwa binadamu huenda wakakabiliwa na kitisho.
Ugunduzi huo mpya wa virusi hivyo umeripotiwa nchini Romania na Russia siku moja baada ya China kusema kuwa imepoteza maelfu kadha ya kuku kutokana na virusi hivyo.
Ujerumani wakati huo huo imeamuru wakulima wake kuwaweka kuku ndani kama njia ya kujikinga.
Hungary inasema kuwa imepata dawa mpya ambayo inaonekana kuweza kuwakinga binadamu na wanyama dhidi ya virusi hivyo.
Umoja wa mataifa umeonya kuwa kuripotiwa kwa kuzuka tena hivi karibuni kwa virusi hivyo kunaongeza uwezekano wa kuenea kwa homa hiyo hatari ya mafua ya ndege hadi katika bara la Afrika pamoja na mashariki ya kati, katika njia wanayopitia ndege wanaohama hama.